Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia – Arusha.
Katika kipindi ambacho Tanzania na nchi nyingine za Afrika zinaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Shirika lisilo la kiserikali la Media for Environment, Science, Health and Agriculture (MESHA) limetoa mafunzo kwa njia ya mtandao kwa waandishi wa habari kutoka nchi sita za Afrika, yakilenga kuimarisha uandishi wa habari za mazingira, kilimo na afya.
Mafunzo hayo yamekuja wakati Tanzania ikishuhudia mabadiliko ya misimu ya mvua, kuongezeka kwa vipindi vya ukame na mafuriko katika baadhi ya maeneo hali inayoathiri uzalishaji wa kilimo, upatikanaji wa maji na usalama wa chakula.
Sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania imeendelea kuwa miongoni mwa sekta zilizo hatarini zaidi kutokana na athari za tabianchi.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa MESHA Aghan Daniel, amesema lengo kuu ni kuwawezesha waandishi wa habari kuandika habari zenye ushahidi, zenye kugusa jamii na zenye kuchochea mabadiliko chanya.
“Mabadiliko ya tabianchi ni suala linalozikumba nchi nyingi duniani, hatuwezi kuzungumzia eneo moja pekee, leo tumepata fursa ya kuwa na wataalamu mbalimbali ili kuwaongezea waandishi uelewa wa kuandika habari zinazoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii,” amesema.
Kwa upande wake mtaalam wa haki za tabianchi kutoka ActionAid International, Teresa Anderson, amesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa chanzo cha hofu duniani kote kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, kupungua kwa ajira na kuongezeka kwa ajira zisizo salama.
Amesema kuna umuhimu wa kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya kusaidia jamii kukabiliana na hasara na uharibifu unaotokana na majanga ya hali ya hewa pamoja na kuimarisha ustahimilivu kwa athari za baadaye.
“Jamii zinahitaji usaidizi wa kifedha ili ziweze kupona baada ya maafa yanayosababishwa na hali ya hewa, hata hivyo suluhisho lazima liwekwe kwa vitendo na si kubaki kwenye ahadi pekee,” amesisitiza.
Naye Afisa wa masuala ya kiufundi kutoka Africa Center for Health Climate and Gender Justice Alliance, Imali Ngusale, amesema ingawa mabadiliko ya tabianchi huathiri makundi yote, wanawake na watoto huathirika zaidi kutokana na majukumu yao ya kila siku yanayotegemea rasilimali za mazingira kama maji na nishati.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia kuongeza idadi ya habari zenye kina na uchambuzi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, huku yakilenga kuhamasisha uwajibikaji wa sera na hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hiyo barani Afrika.


