Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia misingi ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kutoa taarifa sahihi, zenye uhalisia na kuepuka matumizi ya picha potofu kutoka mitandaoni.

Akizungumza leo Mei 2, 2024 katika Ofisi za TEF jijini Dar es Salaam, Balile alisema waandishi wanapaswa kutumia taaluma yao kikamilifu ili kuhakikisha jamii inapata habari za kweli na zenye ushahidi wa kutosha.

“Waandishi wa habari wanapaswa kuripoti kwa kufuata misingi ya taaluma na kutoa taarifa zenye usahihi. Ni muhimu kutumia vyanzo vya kuaminika na kuepuka kuchukua taarifa bila uchunguzi,” alisema Balile.

Akizungumzia kuhusu kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Balile alieleza kuwa waandishi wa habari wataruhusiwa kuingia mahakamani Mei 6, mwaka huu, siku ambayo kesi hiyo itasikilizwa tena.

“Ni lazima waandishi watambulike kabla ya kuingia mahakamani. Watatakiwa kuwa na kitambulisho maalum cha ofisi au ‘Press Card’ kwa ajili ya uthibitisho,” alisisitiza.

Baada ya zile purukushani pale mahakamani, nikasema haiwezekani mwandishi akazuiwa kufanya kazi yake.

“Nilikutana na Afande Jumanne Muliro (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam) na tukakubalia kuzuia waandishi Kisutu sio jambo jema. Tukakubaliana siku ya kesi ya Lissu tarehe 6 Mei waingie wote lakini kuwe na utambuzi,” alisema.

Balile alisema, mwandishi hapaswi kuzuiwa kufanya kazi yake ya kukusanya, kuchakata na kuhabarisha umma.

Hata hivyo alisema, wanahabari wanapaswa kufika mahakamani mapema kwa kuwa, chumba kikijaa hawatopata nafasi.

Naye mjumbe wa Kamati Tendaji TEF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam ( DPC), Bakari Kimwanga alisema, wanahabari wanapaswa kuhakikisha wanakuwa salama wakati wa kazi.

“Jambo la usalama ni la kwanza kisha kazi (habari), jukumu la usalama ni lako mwanahabari,” alisema.

Katika hatua nyingine, Balile amekemea tabia ya baadhi ya waandishi kutumia picha kutoka mitandaoni ambazo mara nyingine si halisi, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kupotosha umma.

“Mwandishi wa habari unatakiwa kuamini picha uliyopiga mwenyewe badala ya kutegemea picha za mitandaoni ambazo mara nyingine hutengenezwa na hazina uhalisia,” aliongeza.

TEF imeendelea kusisitiza umuhimu wa weledi na maadili ya taaluma ya habari ili kulinda heshima ya tasnia hiyo pamoja na kulinda haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.