📍 Bungeni Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, wameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa juhudi kubwa zinazofanywa kuinua kilimo cha Umwagiliaji nchini kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.

Wajumbe wa kamati hiyo wamesema Tume inastahili heshima na pongezi za pekee zimfikie Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa kwa juhudi kubwa za kukamilisha miradi ya kimkakati ya Umwagiliaji nchini.

Hayo yamebainika wakati wa kikao cha Kamati hiyo ya Bunge na Semina maalumu Mkoani Dodoma, ambapo kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Deodatus Mwanyika (Mb) Njombe Mjini.

Mwanyika amesema, Tume inafanya kazi kubwa na nzuri na mabadiliko makubwa yamefanyika.

Amesema pamoja na hatua hiyo Serikali inahitaji kuwapo na mpango maalumu wa kutenga fedha na kuwa na mkakati wa Kitaifa wa kuiwezesha Tume kwa kuwa na vyanzo vingine vya mapato.

“Ni muhimu Serikali kutafuta vyanzo vipya vyamapato na kuhakikisha Tume inawezeshwa kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati, hatua ambayo itachochea ajira hususani kwa vijana, kukuza uchumi na kuendelea kuimarsiha sekta ya kilimo,” amesema.

Amesisitiza kuwa, Kamati hiyo itaendelea kushirikiana na NIRC ili kuhakikisha malengo ya kitaifa ya kilimo cha Umwagiliaji yanatimia.

Naye Mbunge Mhe. Yustina Rahi Mbunge Viti Mkoa wa Manyara na Mhe. Khadija Hassan Aboud (Mb) Zanzibar, waliipongeza Tume kwa kazi nzuri inayoendelea huku wakihimiza umuhimu wa kulinda maeneo ya Umwagiliaji ikiwemo mabwawa na vyanzo vya maji ili miradi hiyo iwe endelevu na isaidie vizazi vijavyo.

Naye Mhe. Dkt. Ritta Kabati (Mb.) jimbo la Kilolo na Sospeter Muhongo ((Mb) Musoma Vijijini walieleza kufurahishwa na miradi mikubwa ya uwezeshaji, hususan ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkombozi lililopo mkoani Iringa na kusisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaongeza tija ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Kwa upande wake Mhe. Cherehan Peter (Mb), Ushetu alisema kuna mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Tume ili kuimarisha sekta ya kilimo kupitia Kilimo cha Umwagiliaji nchini, hatua ambayo inahitaji kupongezwa na kuungwa mkono.

Kwa upande wa Tume, akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji kwa kamati hiyo ya Bunge, Mkurugenzi Mkuu Bw.Mndolwa amesema, Tume imekuwa chachu ya mageuzi ya kilimo cha Umwagiliaji, ikichochea uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, na kuchangia kwa kasi katika maendeleo ya viwanda na biashara nchini.

Mndolwa ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt,Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiwango kikubwa kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ili kuinua mchango wa kilimo katika pato la Taifa.

Amesisitiza kuwa, Serikali imefanya uwekezaji wa jumla ya trilioni 6.6 kwa ajili ya ujenzi wa miradi na ununuzi wa vifaa kwa lengo la kuhakikisha kilimo cha Umwagiliaji kinakuwa nguzo ya kilimo nchini na kuchangia kukua kwa pato la Taifa na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Amebainisha kuwa usanifu wa miradi 26 mikubwa na ya kandarasi yenye thamani ya shilingi trilioni 4.1 umekamilika, ikihusisha mabonde ya mto Ngono, Kaboroboro, Rufiji na Ikamasambo.

Ameongeza kuwa, usanifu wa mradi mkubwa wa Umwagiliaji wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria na Tanganyika unaendelea na unakadiriwa kugharimu shilingi trilioni 2.5.
Mndolwa amesema kuwa uwekezaji huo unalenga kuongeza tija ya kilimo na kupunguza utegemezi wa mvua, huku ukihakikisha usalama wa chakula na mchango wa kilimo katika pato la Taifa unaongezeka kwa kasi.

Amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuimarisha ajira kwa vijana na wakulima wadogo.

Kwa mujibu wa Mndoilwa, Katika utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji , Tume imenunua vifaa mbali mbali kwaajili ya utekezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ikiwemo Magari 63 ya kazi na usimamizi, Mitambo 30 ya ujenzi, Magari makubwa 18 ya kubeba mizigo, Mitambo 19 ya uchimbaji wa visima virefu na piki piki 23.

Amesema mbali na uwekezaji huo, Serikali pia imewezesha ununuzi pampu 1000 za kuteka maji ziwani (surface water pumps) ambazo zimesambazwa katika mikoa ya Mwanza (179), Geita (141), Kagera (133), Mara (100), Simiyu (100), Kigoma (100), na Katavi (100). Hatua hii inalenga kuongeza upatikanaji wa maji ya Umwagiliaji na kukabili changamoto za ukame katika maeneo yenye fursa kubwa za kilimo. ‎