Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametoa wito kwa Serikali kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo na bajeti za taifa zinazingatia hali halisi ya maisha ya wananchi na muktadha wa ndani badala ya kufuata mifumo ya maendeleo ya mataifa ya nje.

Hayo yamejiri leo June 13,2025 Bungeni Dodoma wakati wa mjadala wa Bajeti kuu ya Serikali ambapo Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukuru Manya, amesema mijadala ya ukuaji wa uchumi mara nyingi imekuwa ikiegemea kwenye takwimu bila kuangalia hali ya maisha ya wananchi.

Amesema Pato la Taifa linaweza kuongezeka bila kugusa maisha ya watu wengi, na hilo linaibua swali la “thamani hiyo inamilikiwa na nani!

“Tunatakiwa kuweka thamani hii mikononi mwa Watanzania wenyewe,” amesema Prof. Manya, na kusisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuwa wamiliki na wanufaika wa uchumi wao.

Ametumia nafasi hiyo pia kushauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye tafiti, sera na mikakati inayolenga kupunguza pengo la kipato na kuwezesha maendeleo jumuishi.

Naye Mbunge wa Musoma Vijijini,Prof Sospeter Muhongo (CCM)amesisitiza umuhimu wa wataalamu kuandaa sera na mipango kwa kuzingatia mazingira halisi ya maisha ya Watanzania badala ya kuiga mifumo ya nchi zilizoendelea.

Amesema haina maana kutumia mikakati ya kiuchumi ya mataifa makubwa kwa hali ya Tanzania na kuongeza kuwa licha ya uchumi wa Tanzania kukua tangu miaka ya 2000, bado ukuaji huo haujaakiasi kupunguza umaskini.

“Ndoto ya kufikia uchumi wa kati au wa juu lazima iendane na mipango shirikishi inayotambua kuwa hali ya wananchi bado ni ya kipato cha chini,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mbunge wa Kuteuliwa, Balozi Dkt. Bashiru Ally, ameelezea kushangazwa na kutokuwepo kwa wawakilishi wa Wizara ya Fedha kwenye mjadala muhimu wa masuala ya kodi, jambo alilolitaja kuwa ni upotevu wa fursa kwa taifa kueleza mikakati yake ya mapato ya ndani.

“Tulitegemea watu wa Wizara ya Fedha wawepo kwenye mjadala huu kwa sababu tunaongelea ushuru wa kodi na namna ya kukuza uchumi,” anasema

Dkt. Bashiru ameelezea mafanikio ya Bunge la Kumi na Mbili katika kuwekeza kwenye sekta za elimu, afya, na miundombinu, akisema mafanikio hayo yanapaswa kuwa dira ya kupanga vipaumbele vya miaka ijayo.

Hata hivyo, amekosoa uwepo wa vipaumbele visivyopimika au visivyoendana na malengo ya kitaifa, akisema hali hiyo inasababisha kupoteza rasilimali na kuongeza kuwa bajeti na mipango lazima zijikite katika utafiti wa kitaalamu na si mazoea .

Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba (CCM), naye alikosoa hali ya uendeshaji wa uchumi wa rasilimali ambapo alitoa mfano wa sekta ya uvuvi katika Ziwa Victoria, akieleza kuwa wachina huvua hadi samaki laki tano kwa siku huku wavuvi wa ndani wakishindwa hata robo yake.

Amesema hali kama hiyo pia inaathiri wakulima na wafugaji wadogo wanaoshindwa kushindana na wawekezaji wakubwa kutoka nje.

“Tunazungumza juu ya kukuza uchumi lakini hatuoni faida kwa Watanzania wa kawaida,Samaki wanaofugwa kwenye vizimba ziwani wanapewa dawa ili wasizae, chakula wanachopewa kinawazuia ,wataalamu wetu wamefanyia hili utafiti kweli?” alihoji.

Mbunge huyo ameshauri viwanda vya ndani kutumia mazao ya wakulima kama miwa, tangawizi, na matunda kutengeneza bidhaa kama vinywaji vya nishati, badala ya kuagiza malighafi kutoka nje.

Kutokana na hayo Serikali kupitia Tume ya Mipango imeeleza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) unaolenga kukuza uchumi jumuishi na shirikishi.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Fred Matola Msemwa ameeleza kuwa mpango huo umelenga kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi na shirikishi kwa kuimarisha sekta muhimu kama viwanda, sayansi, teknolojia, biashara na uwekezaji.

Ameitaja Miradi mikubwa kama SGR, umeme wa Julius Nyerere, Daraja la Kigongo–Busisi na bomba la mafuta ghafi (EACOP) kuwa katika hatua za juu za utekelezaji na kwamba Uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika kwa wastani wa asilimia 5.5 huku mapato ya ndani yakifikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa.

Pia ametaja mafanikio katika sekta za viwanda, madini, utalii, elimu na maji, huku ikifuta tozo 374 ili kurahisisha mazingira ya biashara.

Aidha, idadi ya watalii imeongezeka hadi milioni 2.14, bidhaa za viwandani zimechangia asilimia 39 ya mauzo nje, na kiwango cha utoshelevu wa chakula kufikia asilimia 128.

Hata hivyo amebainisha changamoto kama kutotimia kwa baadhi ya malengo, ushiriki mdogo wa sekta binafsi, pengo la ujuzi na upungufu katika muunganiko wa sekta kuwa zimechukuliwa kuwa msingi wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.