Rais wa Wachimbaji Madini, John Bina, amesema kuwa wachimbaji zaidi ya 250 wamemhakikishia kuwa watamchagua Oktoba 29 kwa sababu amewaheshimu. Aidha, amebainisha kuwa hapo zamani familia zilikuwa na hofu kwamba kijana akiwa mchimba madini anapotea.
Ameyasema hayo Oktoba 13, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizofanyika katika Viwanja vya EPA Bombambili mjini Geita.
Aidha, amebainisha kuwa msema ukweli ni mpenzi wa Mungu, na kwamba anazungumza kwa niaba ya wachimbaji wote wa madini nchini. Ameongeza kuwa wachimbaji wamemwahidi Dkt. Samia kuwa watamkinga kwa wivu na kwa gharama yoyote.
Amesema kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utulivu. Vilevile, amebainisha kuwa wachimbaji madini wamepongeza hali hiyo ya amani na wameuliza kwa nini nchi isiige mfano wa Dubai katika kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi.
Aidha, amesema kuwa wachimbaji watampigia kura Dkt. Samia kwa sababu amewapa leseni zisizo na mipaka. Pia, amebainisha kuwa wanahitaji wawekezaji zaidi, na anaamini kuwa chini ya uongozi wake watapata wawekezaji wengi kama kampuni ya GGM.
Vilevile, amebainisha kuwa serikali ya Dkt. Samia imeondoa kodi zilizokuwa kero kwa wachimbaji, huku akifafanua kuwa idadi ya wanawake wachimbaji imeongezeka na sasa imefikia zaidi ya milioni moja.
Aidha, amesisitiza kuwa watu wanaotaka kuandamana wasipewe nafasi na kumuomba Dkt. Samia kuwazuia, ili kulinda amani ya nchi. Amesema kuwa endapo machafuko yatatokea, wazee na watoto hawatakuwa na pa kwenda, huku akibainisha kuwa wanaohamasisha maandamano wapo nje ya nchi, hususan Marekani.
Mwisho, amebainisha kuwa wananchi wa Geita, wachimbaji na wananchi kwa ujumla wamemwahidi kumpigia kura za “NDIYO” Dkt. Samia ifikapo Oktoba 29.
