Na Mwandishi Wetu,JamhurMedia
Dar es Salaam

Wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji, matumizi ya teknolojia duni ya uchimbaji, elimu ndogo kuhusu usalama na utunzaji wa mazingira, pamoja na ugumu wa kupata leseni za uchimbaji.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Matukio wa taasisi ya Green Mining Awareness, John Paul, Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa suluhisho la changamoto hizo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali katika mkutano utakaofanyika Aprili 17, 2026 wilayani Chunya, mkoani Mbeya.

“Serikali na wadau wanajitahidi kutatua changamoto hizi kwa kutoa mafunzo na kuendesha kampeni kama Green Mining Awareness, kwa lengo la kuboresha sekta hiyo na kujenga uchumi kwa wachimbaji wadogo wenye kipato cha chini,” amesema Paul.

Ameeleza kuwa ukosefu wa mitaji na mikopo unawalazimu wachimbaji kutumia mbinu duni za uchimbaji kama mnembe, pamoja na matumizi holela ya kemikali hatarishi kama zebaki (mercury) bila utaalamu, hali inayohatarisha afya, kuharibu mazingira, kupunguza uzalishaji na kuongeza hatari ya ajali migodini.

Katika mkutano huo, taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya NMB zinatarajiwa kutoa elimu na suluhisho kuhusu changamoto za ucheleweshaji wa leseni na upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji.

Licha ya juhudi za Serikali kuendelea kutoa elimu, kurahisisha upatikanaji wa leseni na kuwahamasisha wachimbaji kujiunga katika vikundi ili waweze kufikiwa na mikopo, bado kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi katika utekelezaji wake.

Aidha, taasisi mbalimbali zikiwemo benki, kampuni za vifaa vya uchimbaji kama RM Kyando na Kaeser Compressor zinatarajiwa kushiriki, zikitoa fursa kwa wachimbaji kupata elimu ya namna ya kununua au kukopeshwa vifaa kwa njia sahihi ili kuboresha shughuli zao.

Kwa upande wake, Balozi wa taasisi hiyo, Anna Nyange, amesema mkutano huo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika kujenga sekta ya madini iliyo endelevu na yenye manufaa kwa wote.

“Naamini wadau wengi watajitokeza katika mkutano huu wenye fursa za elimu, teknolojia na mitandao ya kibiashara, ambapo wachimbaji watakutana na wafanyabiashara mbalimbali ili kupata njia sahihi za kufanikiwa,” amesema Nyange.

Aidha, kupitia kampeni zake, taasisi ya TWC inaendelea kuhamasisha wachimbaji kuachana na mbinu hatarishi na kuingia katika uchimbaji rafiki wa mazingira (Green Mining).