Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WADAU wa kilimo mseto Tanzania Bara, wameishauri serikali kupitia wizara tano mtambuka, kutenga bajeti kwa ajili ya kilimo ambacho kinaonesha kuwa na matokeo chanya kwa wakulima wadogo.

Ushauri huo umetolewa na wadau hao waliokutana kwa siku moja jijini Dodoma kupitia, kuchambua na kujadili Bajeti za Wizara tano ambazo zinahusika na kilimo moja kwa moja.

Wizara hizo ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano.

Akizungumza wakati wa kutoa mapendekezo ya wadau hao, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Civic Social Protection Foundation (CSP), Nemence Iriyo amesema wamekuwa wakifanya uchambuzi wa bajeti mara kwa mara na kuishauri serikali, hivyo wameona kwa sasa watoe ushauri kwenye bajeti za wizara hizo tano.

Amesema CSP chini ya ufadhili wa ufadhili wa Vi Agroforestry imekutanisha wadau wa kilimo mseto kujadili, kuchambua na kutoka na mependekezo ambayo yanaweza kutumiwa na watunga sera na wafanya maamuzi katika wizara hizo tano ambazo zinahusika na sekta ya kilimo kwa njia moja au nyingine.

Mkurugenzi huyo amesema kikao hicho cha wadau kimetoa mapendekezo 12 ambayo wanashauri serikali kuyatekeleza kwa maslahi ya kilimo mseto.

“Kwa takribani miaka mitano sasa tunaona bajeti za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Mazingira zimekuwa zikiongezeka na Wizara ya Maliasili na Utalii ikishuka, huku ikitakiwa kusimamia Mkakati wa Kitaifa wa Kilimo Mseto nchini, ila pamoja na kuongezeka kwa bajeti hizo bado kilimo mseto hakijapewa msukumo,” amesema.

Iriyo amesema Bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2021/22 ilikuwa zaidi ya Shilingi bilioni 294, 2022/23 Shilingi bilioni 751, 2023/24 Shilingi bilioni 970, 2024/25 Shilingi trilioni 1 na 2025/26 Shilingi trilioni 1.2, hiyo ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 379.

Mkurugenzi huyo alisema ongezeko hilo limeonekana TAMISEMI kutoka shilingi trilioni 7 hadi shilingi trilioni 11 sawa na ongezeko la asilimia 34 na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kutoka Shilingi bilioni 28 mwaka 2021/22 hadi Shilingi bilioni 81 sawa na ongezeko la asilimia 383.

“Wizara ya Mifugo na Uvuvi bajeti imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 169 hadi Shilingi bilioni 476 sawa na ongezeko la asilimia 223 na maliasili kutoka Sh bilioni 571 hadi 359 sawa na ongezeko asilimia 31,” amesema.

Amesema uchambuzi huo umewapa picha halisi ambayo imeonesha kuwa pamoja na wizara hizo kutenga bajeti kila mwaka ila eneo la kilimo mseto halijapewa kipaumbele kikubwa, hivyo wanaomba serikali kuangalia upya bajeti zake ili ziwe na tija.

Mratibu wa Mtandao wa Bayoanuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, wanapendekeza serikali kutengea asilimia 10 ya bajeti ya wizara ya kilimo kama Azimio la Malabo linavyotaka.

“Utekelezaji kilimo mseto unahusisha wizara takribani tano kama ambavyo zimeanishwa, hivyo tunapendekeza mipango ya wizara hizo isomane, ili kuepusha kuleta tija kwenye sekta ya kilimo,” amesema.

Amesema wizara zinapaswa kuweka fungu maalumu ambalo litawezesha utekelezaji mkakati wa kilimo mseto unaosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Pia wameshauri mipango na mifuko mbalimbali ikiwemo wa misitu inakuwa na kipengele cha kilimo mseto ili kuweza kutekeleza mkakati wa kilimo hicho.

Mratibu wa Mradi wa Kilimo kwa Lishe Bora, Edina Mwasile amesema eneo lingine ambalo wanashauri serikali ni kuimarisha uratibu kwa idara za kilimo, mifugo, misitu, maliasili na mazingira, ili kilimo mseto kiweze kukua.

“Kilimo mseto kinaweza kufanikiwa iwapo viongozi kuanzia vijiji na halmashauri wataelewa dhamira na mikakati ambayo ipo,” amesema.

Pesa Kusaga kutoka Shirika la PELUM Tanzania, amesema serikali ina wajibu wa kuandaa muongozo wa kilimo mseto, ili kuonesha njia sahihi ya utekelezaji kupitia maofisa ugani.

Kusaga amesema pia serikali inatakiwa kuhamasisha upandaji miti mipakani mwa mashamba, ili kilimo mseto kiweze kuonekana kivitendo.

“Serikali inatakiwa kutoa motisha kwa wakulima ambao wanatekeleza kilimo mseto, kwa kuwapatia ruzuku za kilimo,” amesema.

Aidha, wadau hao walipendekeza kufanyika mapitio ya sera ili kuhakikisha kilimo mseto kinajumuishwa vizuri na kuleta ufanisi.

Pia waliomba Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kutengeneza muomgozo wa hewa ukaa ambao utatoa mwelekeo wa ushiriki wa wananchi na kuwapatia faida endelevu.