Zaidi ya wadau 100 wa sekta ya bandari na usafirishaji wameeleza matarajio yao juu ya maboresho ya uendeshaji wa bandari kwa lengo la kupunguza gharama za biashara na kuhakikisha manufaa yanawafikia wananchi kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP).

Wadau hao walikutana jijini Dar es Salaam katika mkutano uliohudhuriwa na taasisi za serikali, mamlaka za bandari na usafiri, sekta binafsi ya usafirishaji, waagizaji, wauzaji nje pamoja na wamiliki wa mizigo, wakijadili ufanisi na uendelevu wa bandari za Tanzania.

Katika mjadala huo, ilielezwa kuwa bado zipo changamoto katika mnyororo wa biashara na usafirishaji zinazohitaji kuendelea kufanyiwa kazi, ikiwemo gharama za usafirishaji na ufanisi wa huduma, ili kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania kikanda.

Wadau walibainisha umuhimu wa Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa kuimarisha mifumo ya PPP, ili rasilimali za bandari zitumike kwa tija na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa pamoja na ustawi wa wananchi.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ushirikiano wa Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, alisema sekta ya bandari na usafirishaji ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa na ina nafasi kubwa ya kuongeza mchango wake endapo uwekezaji utaendelea kufanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.