Na Mwandishi Wetu
WADAU wametakiwa kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha agenda ya mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira inakuwa sehemu ya vipaumbele katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Dkt. Paul Deogratius aliyemwakilisha Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kufanya Mapitio ya Rasimu ya Dira ya Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Uzalishaji wa Gesijoto iliyofanyika jijini Dodoma .
Dkt. Paul alisema kikao kazi hicho ni hatua muhimu katika maandalizi ya Mkakati, kikilenga kuhakikisha Dira na Mpango Kazi ni wa vitendo, unaotekelezeka na unaoendana na vipaumbele vya kitaifa.
Aliwahimiza wadau kutambua fursa na changamoto zilizopo katika sekta na mipango ya kitaifa, kuimarisha uratibu wa kitaasisi na uwezo wa utekelezaji pamoja na Kukuza usawa na ujumuishaji wa makundi yote ya jamii katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema mabadiliko ya tabianchi yana athari kubwa kwa afya ya binadamu, mifumo-ikolojia, uchumi na ustawi wa jamii na kuleta athari zikiwemo kuongezeka kwa ukame kunakoathiri upatikanaji wa chakula, maji na malisho ya mifugo.
Dkt. Paul alitaja athari zingine kuwa ni mafuriko, kuyeyuka kwa barafu katika vilele vya milima mirefu, kama vile Mlima Kilimanjaro, kunakoathiri upatikanaji wa maji na vivutio vya utalii pamoja na kuongezeka kwa ujazo wa maji ya bahari, hivyo kusababisha kuingia kwa maji chumvi katika maeneo ya mwambao na kuathiri upatikanaji wa maji safi, kuathirika kwa miundombinu na ardhi ya kilimo kutokana na ongezeko la maji chumvi.
“Hali hii inahitaji hatua madhubuti na za kimkakati. Mathalani, hali ya hewa ya Dodoma imebadilika katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kipindi hiki kilipaswa kuwa cha masika tofauti na hali tunayoshuhudia. Aidha, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sekta zote za kiuchumi na kijamii. Athari za mabadiliko ya tabianchi inakadiriwa kuligharimu Taifa letu hadi kiasi cha asilimia 3 ya Pato la Taifa kwa mwaka,” alisema.
Aliongeza kuwa Dira ya kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Uzalishaji wa Gesijoto inalenga kufanikisha maendeleo ya kiuchumi sanjari na kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kuimarisha ustahimilivu ambapo mchakato huo utanufaika na maandalizi yanayoendelea ya Dira ya Taifa 2025 ambapo moja ya nguzo tatu za utekelzaji wake ni Hifadhi ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi. Hivyo, Mkakati huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa malengo ya muda mrefu ya Dira ya Taifa 2050 yanawekewa msingi imara wa kuyafikia.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Bw. Thomas Chali kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mazingira alisema kutokana na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na ongezeko la uzalishaji wa gesijoto duniani, Jumuiya ya Kimataifa imeanzisha mikataba ya kimataifa kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ukiwemo Mkataba Mkuu ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) wa mwaka 1992 Tanzania iliridhia mkataba huu Aprili, 1996.
Alisema katika kuwezesha utekelezaji wa Mkataba huu, mikataba midogo miwili ilianzishwa chini yake ikiwemo Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris ambapo Itifaki ya Kyoto ya mwaka 1997 inalenga kuziwajibisha nchi zilizoendelea ambazo ni wazalishaji wakubwa wa gesijoto, kupunguza kiwango cha uzalishaji wake ikilinganishwa na viwango vya uzalishaji kabla ya mwaka 1990.
Tanzania iliridhia Itifaki ya Kyoto mwaka 2002. Vile vile, Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 yana lengo la kushirikisha Nchi zote Wanachama katika juhudi za upunguzaji wa gesijoto na kusaidia nchi zinazoendelea kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia upatikanaji wa rasilimali fedha na teknolojia. Tanzania iliridhia Makubaliano ya Paris mwaka 2018.
Hivyo, Bw. Chali alisema kulingana na Ibara ya 4.19 ya Makubaliano ya Paris, Nchi Wanachama zinapaswa kuandaa na kutekeleza Mikakati ya Taifa ya Kupunguza Uzalishaji wa Gesijoto (LTS). Mkakati huu ni nyenzo muhimu ya kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuimarisha uhimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi.


