Waedesha mashitaka wa umma katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameomba rais wa zamani wa taifa hilo Joseph Kabila kupewa adhabu ya kifo katika kesi inayomkabili ya uhaini.
Kabila anashitakiwa bila kuwepo mahakamani kwa makosa hayo na mengine ya uhalifu wa kivita, yanayohusishwa na uongozi wake wa takriban miaka 20 katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Kabila aliyoiongoza Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, alifunguliwa mashitaka tangu mwezi Julai yanajumuisha pia mauaji na ubakaji.
Serikali ya Kongo pia imedai kiongozi huyo wa zamani analiunga mkono kundi la M23 linalodhibiti miji miwili muhimu nchini humo ya Goma na Bukavu.
Hakuna tarehe rasmi iliyotolewa ya kutoa uamuzi wa mahakama juu ya kesi hiyo.
Kabila alichukua madaraka akiwa na miaka 29 baada ya baba yake Laurent Kabila kuuwawa na kurefusha uongozi wake kwa kuchelewesha uchaguzi kwa miaka miwili baada ya muda wake kumalizika mwaka 2017.
