Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAFANYABIASHARA Jiji la Dar es Salaam, wameeleza kufarijika na hatua za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha mfumo wa kodi na sheria za biashara, wakisema zimesaidia kupunguza gharama na kuondoa changamoto zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 13, 2025 jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo na Taifa, Award Mpandilah, amesema mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Rais Samia yamewapa nguvu mpya ya kuendeleza biashara kwa uhuru na ustawi.

“Kwa muda mrefu kodi ya VAT ilikuwa mzigo mkubwa kwetu. Tulipambana bila kuona mwanga wa suluhisho, lakini sasa kiwango cha mauzo kinachotozwa VAT kimepandishwa kutoka milioni 100 hadi milioni 200. Hii ni hatua kubwa na tunaiomba serikali ikifikishe hata milioni 500,” amesema Mpandilah.

Amefafanua kuwa, awali wafanyabiashara walipata hasara kubwa kutokana na faini za mizigo iliyotoka nje bila kukaguliwa kwenye chanzo cha uagizaji.

“Faini ya milioni 15 ilitupa majeraha makubwa. Tuliona tunafanya kazi kwa hasara. Lakini marekebisho yaliyofanyika yamepunguza mzigo huu kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Aidha, amesema marekebisho ya adhabu kwa makosa ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD) kutoka milioni 4.5 hadi milioni 1.5 kwa kosa yamekuwa mkombozi.

“Fikiria kosa la kutotoa risiti ya shilingi 2,000 kupelekea faini ya mamilioni. Hilo lilikuwa balaa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati,” amesema kwa msisitizo.

Mpandilah ameiomba serikali kuhakikisha wanaosimamia kanuni na sheria za kodi wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi.

“Matamanio ya Rais Samia kwa wafanyabiashara ni mazuri, lakini utekelezaji wake unategemea uaminifu wa wasimamizi. Wakitimiza wajibu ipasavyo, biashara zetu zitaendelea kustawi na kuleta tija nchini,” amesema.

Naye, Mfaume Fadhili amesema wamepata manufaa makubwa ya kiuchumi na kisheria kutokana na mabadiliko yaliyofanywa.

“Zamani, mtu mwenye mauzo ya kati ya milioni 100 na 500 alilazimika kumwajiri mhasibu kwa gharama kubwa. Sasa sheria inamruhusu kutengeneza mahesabu kwa mhasibu wa gharama nafuu au hata yeye mwenyewe kama ana ujuzi. Hii imetusaidia kupunguza gharama,” amesema Mfaume.

Ametaja Tume ya Usuluhishi wa Masuala ya Kodi kama chombo kilichosaidia kutatua zaidi ya malalamiko 230 yaliyowasilishwa, na sheria mpya inayozuia wageni kufanya biashara 15 na kufanywa na wazawa pekee.

Kwa pamoja, wafanyabiashara hao wameahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita, wakisisitiza kuwa maboresho hayo yamewapa matumaini ya kuendesha biashara kwa faida na kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa.