Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata taratibu za utumishi wa Umma hii ikiwa ni pamoja na kuwa na weledi na nidhamu ya kazi.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule wakati akifungua mkutano wa tatu wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi hiyo.

Mhe. Mtambule alisema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa wagonjwa ndani na nje ya nchi ni muhimu wafanyakazi hao wakakumbuka kufuata maadili ya kazi zao ili sifa iliyopo ibaki kama ilivyo.

Katibu wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) aliyemaliza muda wake Abdulrahman Muya akimkabidhi nyaraka za utendaji kazi Katibu mpya wa baraza hizo Adam Sembe aliyechaguliwa katika katika  mkutano wa tatu wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

“Sisi kama viongozi wa Serikali na Wananchi tunajivunia kuwa na taasisi hii ambayo inatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na kuokoa maisha ya wagonjwa, hospitali hii ni moja ya vivutio vya utalii tiba vilivyopo hapa nchini”.

“Ninawapongeza kwa kufungua matawi yenu mengine Oyster bay na Kawe, kuwepo kwa kliniki hizi kumesaidia watu wengi zaidi kufikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa  haraka zaidi”, alisema Mhe. Mtambule.

‘Ninampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya afya hii ikiwa ni pamoja na kununua vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalamu wabobezi jambo lililosababisha wananchi wengi kupata huduma za kibingwa za matibabu ndani ya nchi”,  

Aidha Mkuu wa Wilaya hiyo alisema wilaya ya Kinondoni itazidi kushirikiana na taasisi hiyo kwa kufanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo ili wananchi wengi wapate huduma za elimu, uchunguzi na matibabu ya moyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwashukuru wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kujitoa na kuwaomba kuendelea kuwa moyo wa huruma kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule zawadi kutoka kwa taasisi hiyo mara baada ya kufungua mkutano wa tatu wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge alisema moja ya mafanikio ya kujivunia yaliyopatikana katika taasisi hiyo ni kuwepo kwa huduma ya kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkopa ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ambapo hadi sasa imeshawafikia wananchi zaidi ya 22,000.

“Baadhi ya wananchi tuliowaona tuliwakuta na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kuwapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu, kuna ambao wametoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi tunashukuru tumeweza kuokoa maisha yao”, alisema Dk. Kisenge.

Naye Afisa wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Vaileth Ndeza alisema mabaraza ya wafanyakazi yanaratibiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo na kutoa pongezi kwa taasisi hiyo kutekeleza matakwa ya sheria kwa kuwa na mkataba unaounda baraza la wafanyakazi.

“Siku ya leo JKCI imezindua baraza jipya la tatu la wafanyakazi nimewafundisha wajumbe wapya wa baraza wajibu wao ambao ni kumshauri mwajiri juu ya hatua za kuongeza tija na ufanisi katika kutoa huduma na kumshauri mwajiri juu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za utumishi”.

Baadhi wa wajumbe wa  baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiimba wimbo wa “solidarity forever” wakati wa ufunguzi wa mkutano wa baraza la tatu la wafanyakazi wa Taasisi hiyo.

“Kumshauri mwajiri juu ya mambo muhimu yanayohusu maslahi ya wafanyakazi, mazingira ya kazi, upatikanaji wa vitendea kazi, mawasiliano bora sehemu za kazi posho za wafanyakazi na kupokea, kujadili na kuthibitisha mipango ya makisio ya mapato na matumizi ya taasisi” alisema Vaileth.

Vaileth aliwataka viongozi wa baraza hilo kufanya vikao hivyo mara kwa mara kwa kutekeleza matakwa ya kisheria na kusema kuwa taasisi nyingi zimekuwa zikiunda mabaraza ya wafanyakazi lakini wameshindwa kufanya mikutano kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule akizungumza na wajumbe wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) mkoa wa Dar es Salaam Edward Mwashitanda alisema ni muhimu wafanyakazi wa taaasisi hiyo wakawezeshwa maslahi yao kwani wanafanya kazi kwa uweledi na utaalamu wa hali ya juu wa kuokoa maisha ya wagonjwa.

Mwashitanda alisema anaamini baraza hilo la wafanyakazi litaleta mabadiliko katika taasisi hiyo kwa kuendelea kushirikiana kitaalamu katika kutoa huduma nzuri na bora kwa wananchi.