Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KAMPUNI inayoongoza kwa huduma za usafiri mtandaoni nchini, Bolt Tanzania, imeandaa futari na chakula cha mfungo wa Kwaresima kwa zaidi ya madereva washirika 100 katika ukumbi wa Masaki Wellspring Hub, ikiwa ni hatua ya kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wiki chache baada ya maandamano ya baadhi ya madereva yaliyofanyika Februari kuhusu viwango vya makato na muundo wa punguzo la nauli.

Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita iliwakutanisha pamoja madereva na viongozi wa kampunina kushiriki chakula na kufanya mazungumzo. Uongozi wa kampuni ulieleza kuwa mkutano huo umechangia kufafanua masuala yanayohusu upangaji wa bei, kanuni za usafiri, makato na mfumo wa punguzo la nauli. Madereva walipata fursa ya kuuliza maswali moja kwa moja huku menejimenti ikiahidi kushughulikia hoja muhimu zilizowasilishwa.

Ingawa kundi dogo la madereva liliandamana mwanzoni mwa Februari 2026, wiki chache kuhusu viwango vya makato na muundo wa punguzo la nauli lakini pia ushiriki wa chakula cha Pamoja na kufanya mazungumzo ambapo katika hafla hiyo ulionyesha dhamira ya pamoja ya kujenga uaminifu, heshima na mshikamano kati ya madereva na kampuni kinara wa sekta ya usafiri wa mtandao nchini.

Akizungumza wakati wa futari, Meneja Mkuu Mwandamizi wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, alisema kipindi cha Ramadhani na Kwaresima ni muda wa tafakari na umoja. “Kukaa pamoja kumetupa nafasi ya kusikiliza kwa makini, kuondoa sintofahamu na kuimarisha ushirikiano wetu na madereva. Majukwaa endelevu hujengwa kupitia mazungumzo, si kwa kutengana,” alisema.

Madereva walioshiriki walieleza kuwa majadiliano hayo yalikuwa yenye kujenga, yakisaidia kuweka bayana masuala ya upangaji wa bei na matarajio ya mapato ya muda mrefu.

Kwa mujibu wa kampuni, kuunganisha futari na chakula cha mfungo wa Kwaresima pia ni ishara ya Bolt kuzingatia tamaduni na dhamira na kuwa wazi na jumuishi kama mtoa huduma mkuu wa usafiri mtandaoni hapa nchini Tanzania.