Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

WAGANGA wa Jadi Mkoani Tabora wametakiwa kujiepusha na vitendo vya aina yoyote vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Onyo hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora, Komredi Mohamed Katete katika kikao cha siku moja cha Waganga wa Jadi wa Manispaa ya Tabora cha kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusiana na kazi yao.

Alisema kuwa waganga wa tiba asilia (jadi) wana mchango mkubwa katika ustawi wa jamii mahali walipo lakini baadhi yao wamekuwa wakifanya shughuli kwa mihemko hali inayopelekea chuki na uhasama kuibuka miongoni mwa wanajamii.

‘Kila mganga wa tiba asilia akitekeleza shughuli zake kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria zinazowaongoza na kuzingatia miiko ya kazi yao, chuki, uhasama na vitendo vya uvunjifu wa amani havitakuwepo’, alisema.

Katete alisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi na serikali yake wataendelea kuwapa ushirikiano ili kufanikisha shughuli zao lakini akatoa onyo kwa wale wote wanaofanya ramli chonganishi au kutumiwa vibaya na wanasiasa ili wapate ubunge, udiwani au cheo chochote.

Katibu wa Umoja wa Waganga wa Jadi Mkoa wa Tabora Jumanne Mpando alisema kuwa kikao hicho ni muhimu sana kwa kuwa kinatoa mwongozo wa nini mganga wa jadi anapaswa kufanya na nini hapaswi kufanya na athari zake.

Alionya kuwa baadhi yao wamekuwa wakikiuka taratibu za kazi zao na wengine hata kufikia hatua ya kulaza wagonjwa katika nyumba zao jambo ambalo ni kinyume kabisa na kanuni, taratibu na sheria za usajili wao.

‘Hili halikubaliki, yeyote atakayebainika kufanya shughuli nje ya taratibu, sheria na kanuni za umoja wao, ikiwemo kutumia viungo vya binadamu atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkono wake’, alisema.

Kaimu Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Tabora Leonard Mzuka aliagiza Viongozi wa Umoja huo kuhakikisha waganga wote wanaotoa tiba asilia katika Manispaa hiyo na Mkoa mzima wanasajiliwa ili watambulike.    

Aidha aliwataka kujiepusha na vitendo vya uvunjaji nazi, vyungu au kumwaga vitu kwenye mapanda njia ya barabara kwa kuwa wanachafua mazingira lakini pia watoto wadogo wanaweza kuviokota na kula wakaathirika kiafya.