Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Arusha

Wiki iliyokwisha nimeitumia kusikiliza upepo wa siasa unavyokwenda hapa nchini. Kwa hakika kugombea iwe ubunge au udiwani ni kazi kwelikweli.

Wagombea simu zao zinapokewa kila zikiita na kila ujumbe wanaujibu. Sitaki kuamini kuwa teknolojia ya akili mnemba imeanza kutumika. Nimeshuhudia picha za baadhi ya wagombea wakiwa wamekaa chini ardhini na wanaoombwa kura wakiwa kwenye viti vyao.

Nimezisikia kauli za wagombea kukutana na wajumbe. Wengi wanatumia lugha za unyenyekevu kweli. Na hata wanapotaka kuwapatia ‘nauli’ wanawabembeleza wakiwaomba hicho ‘kidogo’ wakipokee. Nikiri rushwa ya kwenye uchaguzi sasa imevuka mipaka. Wajumbe pamoja na wigo kutanuliwa, bado wanadai kupatiwa chochote ndipo wapige kura.

Sitanii, wagombea sasa ni watumwa. Wajumbe wanawaambia waziwazi kuwa kama hawatoi chochote nao kura wazisahau. Mwanzo wimbi ilikuwa ni wagombea wanatoa rushwa, ingawa bado wapo wanaokufuru hata sasa, ila mizani imegeuka. Wajumbe wanadai rushwa. Nimeshuhudia wagombea kadhaa ambao wakifika jioni wanalia. Wanasema wajumbe wanawatamkia wazi kuwa kama hawana fedha wasijisumbue.

Naamini elimu ya uraia sasa inapaswa kuenezwa kuanzia kwa wapigakura. Tunapaswa kuwaeleza madhara ya kudai rushwa. Hicho kidogo kinachotolewa cha Sh 10,000, Sh 20,000 au hata Sh 50,000 wajue wanauza maendeleo ya kata na majimbo yao. Ni matamanio yangu wagombea hawa wanapopita kwenye kata na majimbo yetu, ingekuwa wanaulizwa maswali magumu juu ya changamoto za jimbo au kata.

Tusichokifahamu, siku unapoingia kwenye kituturi cha kupigia kura, yule unayemchagua kwa kumpigia kura, unakuwa umehamishia kwake madaraka yako ya kufanya uamuzi, iwe ni kwenye kata au kwenye jimbo. Madiwani na wabunge wao wanalifahamu hili. Ndiyo maana mara kadhaa utawasikia wakisema “wanachi wamenituma”, “kwa niaba ya wananchi wangu…”

Hawa wanakwenda kuingia kwenye vikao vya uamuzi. Hawa wanaingia bungeni au kwenye mabaraza ya halmashauri na kufanya uamuzi kwa niaba yako. Ni haki na wajibu wako ukikutana na diwani au mbunge kumwambia kuwa barabara za mtaani kwenu ni mbovu.

Ni jukumu lako kama mpigakura kumwambia diwani au mbunge kuwa mnadai huduma ya maji (safi na taka), umeme, hospitali, elimu, upimaji wa ardhi, kujengea madaraja na mengine ya aina hiyo.

Mbunge au diwani tukimpatia hoja kama hizi, anazibeba na kuzipeleka kwenye baraza la halmashauri au bungeni na huko ndiko fedha zetu tunazochangia katika mfuko mkuu wa taifa kwa njia ya kodi zinakofanyiwa uamuzi zitumikeje. Diwani au mbunge ni mwakilishi wako katika vikao hivi. Mnapomchangua mnapaswa kumtuma atatue matatizo au changamoto zilizopo kwenye kata au jimbo lenu.

Sitanii, mnaposikia sera za chama kinapoweka mwakilishi wake kugombea udiwani au ubunge, maana yake huyu mnayemchagua ndiye anayekuwa kiunganishi kati ya chama, serikali na wananchi. Kama mna tatizo la usalama, kwamba vibaka wanakaba watu, huyu ndiye anayepaswa kuwasilisha tatizo hili kwa vyombo vya dola kupitia waziri mwenye dhamana na usalama ukaimarishwa.

Ni bahati mbaya kuwa wagombea wengi wanapofika kwa wananchi hawafafanui majukumu yao ni yapi iwapo watachaguliwa. Wananchi wakiwaona wagombea wanawaona kama ATM au msimu wa mavuno.

Watanzania tubadilike. Tuache tabia ya kuwaomba fedha wabunge na madiwani kwani wao jukumu lao ni kutusemea si kugawa fedha kama njugu. Tukilitambua hilo tutachagua wagombea wanaofaa kisha tuwadai maendeleo kifua mbele.

Mwisho, nimeona wagombea kwa sasa wanapiga magoti, wanakaa chini, wanasalimia na hata simu yako ikijipiga bahati mbaya kwake, si muda anakurejea akisema: “Kaka ulikuwa unasemaje, nimeona simu yako?” Natamani uungwana huu walionao wagombea uendelee hata baada ya kuchaguliwa. Baadhi ya madiwani na wabunge wanazifanya siasa zionekane kuwa kichaka cha wahuni kutokana na matendo yao.

Sitanii, tabia za hawa wagombea kugeuka miungu watu baada ya kuchaguliwa zikome katika siasa za Tanzania. Unyenyekevu mnaouonyesha sasa muendelee nao hata baada ya kuchaguliwa. Sisi wapigakura tunawadai maendeleo si malipo kutoka kwenye mishahara yenu. Hili nalo likieleweka, likaungana na wajumbe kuacha tabia ya kudai rushwa, tutashuhudia maendeleo ya kasi kwenye kata na majimbo yetu. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827