Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa kikao cha mwisho cha uteuzi wa wagombea wake wa nafasi za Ubunge na Udiwani kimepangwa kufanyika tarehe 28 Julai, 2025, badala ya Julai 19 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema mchakato wa maandalizi ya uchaguzi ndani ya chama hicho unaendelea kwa mafanikio huku ukihitaji umakini mkubwa kutokana na wingi wa wagombea.
“Leo wengi walitarajia Kamati Kuu ingeketi kwa ajili ya uteuzi, lakini sasa shughuli hiyo imepangwa kufanyika Julai 28. Hili ni zoezi nyeti linalohitaji umakini mkubwa, na ndiyo maana tumeamua kujipa muda zaidi ili tuweze kufanya kazi hii kwa weledi,” amesema Makalla.
Kwa mujibu wa Makalla, vikao muhimu vya maamuzi vitafanyika kuanzia Julai 26 hadi Julai 28, 2025, ambapo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC) itakutana Julai 26, ikitanguliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambacho kitaweka bayana maamuzi ya awali kuhusu uteuzi.
Amesema idadi kubwa ya waliojitokeza kuwania nafasi hizo imepelekea chama kujipa muda zaidi kufanya uchambuzi wa kina.
“Kwa mfano, wagombea wa nafasi ya udiwani ni zaidi ya 27,000, na wale wa ubunge ni zaidi ya 10,000. Kazi ya kuchambua ni kubwa. Tunataka tutende haki, tufanye kwa umakini na kwa utulivu,” amesema.
Ameongeza kuwa bado hakuna mgombea yeyote aliyekatwa na kwamba kikao cha Julai 28 kitafanya maamuzi rasmi ya nani atasonga mbele kwenye hatua inayofuata ya mchakato wa ndani wa CCM.
“Napigiwa simu nyingi kuhusu lini uteuzi utafanyika. Nataka niwaambie, kazi inaendelea kwa hatua makini. Hakuna aliyekatwa bado. Kikao cha Julai 28 kitaamua rasmi nani anasonga mbele,” amesema Makalla.
Aidha, amesema baada ya uteuzi huo, chama kitapanga na kutangaza ratiba ya kura za maoni, hatua muhimu inayofuata katika kuwapata wagombea wa mwisho watakaowania kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Makalla amewahimiza wagombea wote waliowasilisha nia zao kuwa na uvumilivu na utulivu, akisisitiza kuwa chama kimejipanga kutoa wagombea bora, wa kuaminika na wenye sifa za kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
“Wagombea watulie, wa relax wakati tunaendelea na mchakato mpaka tarehe 28,” amesisitiza.
Uteuzi huu ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ambapo CCM kama chama tawala kimesema kitaibua wagombea wake bora kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika ngazi mbalimbali kuanzia serikali za mitaa hadi ngazi ya kitaifa.
