Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita
IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Geita imewakamata wahamiaji haramu 126, ambao ni raia wa Burundi walioingia nchini, kufanya kazi na kuishi kwenye maeneo tofauti kinyume cha sheria.
Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi ,James Mwanjotile, amesema wahamiaji hao wamekamatwa kwa kipindi mwezi Julai 2025, maeneo ya ndani na nje ya mji wa Geita, ambao wote wanashikiliwa na utaratibu wa kuwarejesha makwao unaendelea.
Amesema tatizo la uhamiaji haramu linakua kwa kasi, kwani kwa robo ya mwisho wa mwaka wa fedha 2024/25 walikamata na kuwarudisha makwao wahamiaji 593.

“Hii inadhihirisha kuwa tatizo la uhamiaji haramu linazidi kuwa kubw,a lakini tunaendelea kupambana kuweza kuwadhibiti kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” amesema Mwanjotile.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kiini cha ongezeko la wahamiaji haramu ni fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Geita zinazochagizwa na shughuli za uchimbaji wa madini, kilimo na ufugaji.
Amesema wengi wao ni raia wa Burundi ambao wanaingia kufanya kazi kwa malipo kidogo, hali inayosababisha tatizo la ajira kwa wazawa na hata kuhatarisha usalama nchini Tanzania.
“Kuna athari nyingi sana kiusalama, kwa sababu tunao watu ambao ni wahamiaji haramu huwezi kujua wamekuja kufanya nini hapa.

“Kwenye masuala ya kiuchumi, tunagombania ajira na wageni, kwenye masuala ya kielimu pia Rais ametangaza elimu bure, tusipokuwa makini tutajikuta kuna watu wanajipenyeza”,amesema.
Mwanjotile ameonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kushiriki kuwaingiza nchini wahamiaji kinyume cha utaratibu atachukuliwa hatua kali pamoja na kugharamia taratibu zote za kuwarejesha makwao.
Mmoja wa wahamiaji waliokamatwa, Sanzamahoro Richard amesema maisha magumu nchini Burundi ndio sababu kubwa iliyomsukuma kuja nchini Tanzania kutafuta ajira ili kujipatia kipato cha kujikimu.
“Nimetokea Burundi, nilikuja nchini Tanzania kutafuta maisha, nilifikia Mwatulole (mtaa) na nilikuwa nafanya kazi ya kuuza mayai”, ameeleza Sanzamahoro.
Naye Ndagijimana Erodi kutoka nchini Burundi amesema aliingia nchini Tanzania na kuanza biashara ya kuuza chips katika kituo cha mabasi Geita mjini ili ajipatie kipato cha kujikwamua na umasikini.
Kwa upande wake Bizimana Gerlad amesema alikuja Geita kutafuta maisha lakini yupo tayari kurejeshwa Burundi kwa kuwa hakuna namna nyingine anaweza kufanya badala yake anatii maelekezo ya idara ya uhamiaji.