Wataalamu takribani 200 wa afya ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wamekutana leo jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutumia Akili Mnemba(AI) katika matibabu ya magonjwa ya mfumo wa chakula yanayoathiri jamii kwa kiasi kikubwa.
Kongamano hilo la kwanza linalohusisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda limeratibiwa na Mtandao wa afya wa wataalamu wa Kiislamu (Jamiibora).
Akizungumza katika kongamano hilo siku moja Katibu Mkuu wa Jamiibora,Dk Muhidini Kassim amesema wanajadili mfumo wa chakula kuanzia magonjwa yanavyochunguzwa na kutibiwa na athari mbalimbali ambazo zinatokana na kuchelewa matibabu au kukosekana kwa huduma za kibobezi.
“Kikubwa ni kujadili namna teknolojia inaweza kutumika katika kuboresha matibabu ya afya hususani mfumo wa chakula,kuna ongezeko kubwa la matatizo ya mfumo wa chakula ambayo yanapelekea saratani.
“Tutaangalia teknolojia mpya namna inavyoweza kutumika katika kuchunguza ,kufanya matibabu ,kufanya upasuaji kwa kutumia Akili Mnemba (AI).
Amesema wangependa kuona jamii inalindwa kwa kupata taarifa sahihi na kwa wakati ya namna ya kujikinga lakini pia namna kutafuta tiba na tiba zinazoweza kusaidia.
Ameeleza kuwa mjadala huo utangazia kuweka maazimo yanayoweza kuwasaidia watunga sera na wataalamu wa afya kuungana kwa kwa pamoja kukumbana na athari.
Kwaupande wake Rais wa Chama cha Kitaaluma cha magonjwa wa mfumo wa chakula, Dk Eraldo Komba amesema magonjwa ya mfumo wa chakula hasa ini yamekuwa na athari kubwa ambapo kati ya watu 100, watu wanne wana ugonjwa wa homa ya ini sawa na asilimi nne.
“Hili linatugusa moja kwa moja takwimu za kitaifa na kimataifa watu wengi wanapata magonjwa mengi na wanakufa kutokana na magonjwa haya mfano kuna saratani ya koo ,saratani ya utumbo mpana na magonjwa ya ini yapo hasa hapa Muhimbili,” amesema.
Amesema katika kongamano hilo watajadili namna ya kuepuka magonjwa hayo kwani kuna magonjwa mengine yanatokana na unywaji wa pombe uliokithiri.
