Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea

WIZARA ya Katiba na Sheria, imeanzisha program ya kutoa mafunzo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ambapo wajumbe na mabalozi 2,200 kutoka kata 11 za jimbo la Songea mkoani Ruvuma wamenufaika.

Mafunzo hayo yalifunguliwa jana wilayani hapa na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Damas Ndumbaro na yanatarajiwa kuwanufaika mabalozi na wajumbe wa maeneo mengi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dk Ndumbaro alisema Wizara imeanza kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kumaliza migogoro ili elimu wanayo pata viongozi hao wakaitumie kutatua migogoro kwa njia mbadala.

“Kipekee tumshukuru sana Rais wetu mpendwa Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia mpatiwe mafunzo haya muhimu ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na zaidi mtapatiwa elimu ya utawala bora na ukatili wa kijinsia”, alisema Dk Ndumbaro

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo kama hayo Wilaya ya Madaba mkoani hapa, Dk Ndumbaro alisema yanalenga kumaliza migogoro mbalimbali ya kisheria inayoibuka na ile iliyoibuliwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Aidha, Dk Ndumbaro alisema mbali ya utatuzi wa migogoro pia viongozi hao wapatiwe elimu ya uraia na utawala bora, elimu ya ukatili wa Kijinsia na elimu kuhusu Uchaguzi Mkuu.

Wajumbe na mabalozi wa wilaya ya Songea wakimsikikiza Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro wakati akifungua mafunzo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini, Comrade Mwinyi Msolomi, aliishukuru serikali kwa kutoa elimu hiyo kwa mabalozi kwakuwa elimu hiyo wanayo pewa inaenda kuboresha uongozi katika ngazi ya serikali za mitaa.

Balozi wa mtaa wa Luila shina namba 2, Swaleh Mayonjo alisema kuwa mafunzo hayo yamemuongezea uelewa wa kisheria katika kuwahudumia wananchi anaowaongoza.

Alisema atayatumia mafunzo hayo kuhakikisha ataelimisha wenzake kuhusu namna bora ya kutatua changamoto ya migogoro ambayo alisema siyo lazima ifike mahakamani.

Alisema utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ni jambo jema kwani kutasaidia kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani kwani itakuwa ikitatuliwa kwenye ngazi za chini.

Alisema pamoja na mafunzo hayo pia wamepewa elimu kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktiba mwaka huu na kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza amani wakati na baada ya uchaguzi huo.

“Tumefurahia mafunzo haya kwasababu yamekuja wakati mwafaka kabisa hawa mabalozi na wajumbe zaidi ya 2,200 watakwenda kutoa elimu kwa wananchi na yatakuwa na manufaa kwa wananchi wengi,” alisema