📌Vijiji vyote 763 sawa na asilimia 100 vimeshapata huduma ya umeme Tanga

📌Vitongoji 2,382 sawa na asilimia 52.6 vimeshapata huduma ya umeme

📌Shilingi bilioni 68.5 yawezesha utekelezaji miradi ya REA Tanga

📍Korogwe – Tanga

Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA, wametakiwa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha wananchi.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 31, 2025 wilayani Korogwe na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, wakati akizungumza na Wakandarasi wa miradi ya umeme wanaotekeleza miradi hiyo mkoani Tanga.

“Katika utekelezaji wa miradi hii bado kuna changamoto ya uunganishaji mdogo wa wateja kwa sababu mbalimbali na kufanya miradi hii kutokumalizika kwa wakati, hakikisheni mnaongeza kasi, maarifa ya kuwahudumia wateja na ubunifu ili uunganishaji uweze kuleta tija,” Amesisitiza Mhe. Balozi Kingu.

Katika hatua nyingine, Balozi Kingu amesema mkoa wa Tanga vijiji vyote 763 vimeshapata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA na vitongoji 2,382 kati ya vitongoji 4,531 navyo vimepata huduma ya umeme na kasi kubwa inaendelea ya kuwaungashia wateja katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amemtaka mkandarasi Ok electrical and Electronics Services Ltd na Wakandarasi wengine kuhakikisha wanaongeza kasi ya kupeleka umeme kwa wateja ili wateja wengi wapate huduma hiyo.

“Sisi REA tutaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hii ili iweze kuwa na mchango mkubwa kwa jamii, ” Amesema Mha. Saidy.

Naye, Kaimu Mhandisi Miradi ya REA Mkoa wa Tanga, Mha. Kelvin Melchiad amesema, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 68.5 ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa na wananchi wanapatiwa huduma ya umeme ili kuwapatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wakandarasi waliohudhuria kikao hicho ni mkandarasi Ok electrical and Electronics Services Ltd, Tontan Project Technology Co. Ltd na Transpower Ltd and Whitecity International Contractor Ltd.