Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anaye shughulikia Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, ametoa onyo kali kwa wakandarasi wanaochelewesha kukamilisha ujenzi wa majengo ya Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, akisisitiza kuwa fedha zote za utekelezaji zimetolewa na hakuna sababu ya uzembe.

Ametoa agizo kwa wakandarasi hao kuhakikisha majengo yote yanakamilika kufikia Oktoba 2025, ili kuharakisha mpango wa serikali wa kuwahamishia watumishi wake na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mfumo mmoja wa utendaji serikalini.

Wazir Lukuvi amezungumza hayo leo July 24 , 2025 Jijini hapa wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa majengo ya Wizara ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi wa majengo ya kudumu ya wizara na taasisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba.

Lukuvi amesema, “Tunataka baada ya uchaguzi mkuu, wizara zote ziwe zimehamia Mtumba,

Hakuna visingizio tena,Serikali imetoa fedha, kazi iliyobaki ni utekelezaji. Msisubiri kuambiwa mara ya pili,” amesisitiza Lukuvi wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dodoma

“Tinasisitiza matumizi ya samani za ndani kama ilivyo kwenye mikataba yenu,hii ni fursa ya kuchochea uchumi wa viwanda vya ndani na tunajua zinadumu zaidi kwa muda mrefu,” amesema Lukuvi.

Mradi huo wa ujenzi unahusisha majengo 34 ya wizara na taasisi, ukigharimu kiasi cha shilingi bilioni 738, ambapo hadi sasa asilimia 92.2 ya kazi imekamilika.

Kwa mujibu wa Noeli Mlindwa, Mratibu wa Kikosi cha Kuhamishia Serikali Mtumba, serikali tayari imeshatoa shilingi bilioni 544.7 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ujenzi, na majengo 10 yameshakamilika na kutumika kwa utoaji wa huduma.

Aidha, amesema serikali imetenga shilingi bilioni 66 kwa ajili ya ununuzi wa samani (fanicha) na vifaa vingine vya ofisi, huku msisitizo ukiwekwa kwenye matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi.

Kwa upande wake, Mlindwa alibainisha kuwa Serikali pia inaendelea na mpango wa upandaji wa miti 253,000 kuzunguka mji huo kwa ajili ya kuutengeneza kuwa mji wa kijani na rafiki kwa mazingira.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa TARURA, Mhandisi Benjamini Maziku, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara kilomita 51 katika Mji wa Serikali Mtumba umekamilika kwa asilimia 100, sambamba na ufungaji wa taa za barabarani na kamera za usalama, ambapo majaribio yanaendelea chini ya mkataba wa miaka mitano na mkandarasi.