Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali imeiagiza Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuwachukulia hatua makandarasi wazembe wanaosababisha hasara na athari kwa serikali na wananchi kwa kutokamilisha miradi kwa wakati.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa agizo hilo leo Mei 15, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2025 uliobebwa na kauli mbiu “Ukuaji wa Makandarasi wa ndani; Fursa na changamoto” na kusisitiza makandarasi hao wana wajibu mkubwa kuinua uchumi.

“Ikumbukwe kuwa makandarasi wanaposhindwa kutimiza wajibu wao wanachelewesha wananchi kupata huduma zilizokusudiwa akini na kusababisha hasara kwa Serikali na wananchi kwa ujumla”, amesisitiza Ulega.

Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa wakandarasi kufanya kazi kwa weledi na kuwapongeza baadhi ya wakandarasi wa ndani kwa kufanyakazi kwa uzalendo na hivyo kumaliza miradi kwa wakati.

“Ikumbukwe kuwa Makandarasi wanaposhindwa kutimiza wajibu wao wanachelewesha wananchi kupata huduma zilizokusudiwa akini na kusababisha hasara kwa Serikali na wananchi kwa ujumla”, amesisitiza Ulega.

Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa wakandarasi kufanya kazi kwa weledi na kuwapongeza baadhi ya wakandarasi wa ndani kwa kufanyakazi kwa uzalendo na hivyo kumaliza miradi kwa wakati.

“Hakikisheni mnazingatia weledi na uzalendo katika shughuli za ukandarasi kwa kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vya ubora kulingana na mikataba ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa wakati na thamani ya fedha iliyokusudiwa”, amesisitiza Ulega.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Farida Mawenya ametoa wito kwa Wakandarasi nchini kuepukana vitendo vya rushwa na kuwataka kushindana kwa haki ili kukuza sekta ya ukandarasi na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa makandarasi wazawa kupitia vifungu wezeshi katika Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kanuni zake za Mwaka 2024 ili waweze kukua na kutekeleza sehemu ya miradi mikubwa ya ujenzi na kuwezesha kushindana katika masoko ya nje ya Tanzania.

Akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Bodi, Msajili wa Bodi ya CRB Mhandisi Rhoben Nkori ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2024 bodi ilisajili jumla ya makandarasi 1,812 na hivyo kufanya idadi ya Makandarasi hai waliosajiliwa kufikia 13,596.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho Bodi imesajili miradi 4,691 yenye thamani ya shilingi za kitanzania trilioni 10.472 na pia ilikagua jumla ya miradi 3,581 ambapo miradi 2,092 (58.4%) haikukutwa na kasoro yoyote na miradi 1,489 sawa na 41.6% ilikutwa na kasoro mbalimbali hivyo kutolewa maelekezo stahiki kwa mujibu wa sheria.

Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi ni jukwaa linalounganisha wadau wa sekta hiyo kutoka Serikalini na Sekta Binafsi wakiwemo waajiri, makandarasi, wataalam washauri na wengineo kukutana kwa ajili ya kupeana taarifa, kushauriana, kujitathimini na kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuboresha ufanisi katika shughuli za ujenzi hapa nchini.