Na WMJJWM- Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewataka wahitimu wa Shahada ya Elimu ya Watu wazima na Maendeleo ya Jamii wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuzingatia Sera na Mipango mbalimbali ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996), Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023, Sera ya NGO’s ya mwaka 2001 pamoja na miongozo na mikakati mbalimbali wakati watakapokuwa wanatoa huduma kwa jamii mara baada ya kuhitimu.

Wakili Mpanju ameyasema hayo Juni 15, 2025 wakati wa sherehe ya mahafali ya tano (5) ya Wahitimu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Shahada ya awali ya Elimu katika Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii- Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM – ADEKA) iliyofanyika katika ukumbi wa St.Peters Swaswa.

Amewataka wahitimu hao kwenda kutekeleza kikamilifu Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa Mwaka 2022/23-2025/26 pamoja na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II- 2024/25- 2028/29.

“Mkawe chachu katika kubadilisha mitazamo na fikra za jamii katika kuchochea maendeleo kwenye jamii, ikiwa pamoja na kuhamasisha watanzania kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuitunza miradi ya maendeleo”. amesema Wakili Mpanju

Amesema kuwa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wanahitajika sana katika Taifa kwa kuwa wana mbinu za kubadili fikra kwa jamii hivyo waende wakawatumikie wananchi wawaongoze ili waweze kufanya majadililiano ya kuibua mila na desturi zinazosababisha ukatili wa kijinsia na kuziendeleza Mila zenye faida kwa jamii.

Aidha, amesema kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kuboresha Sekta ya Maendeleo ya Jamii na hadi Juni 2025, imeajiri Wataalam wa Maendeleo ya Jamii zaidi ya elfu moja na kufanya ongezeko la wataalam hao walioajiriwa hadi Juni, 2025 kuwa 3,976 kutoka wataalam 5,296 wanaohitajika.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Ndaki ya Elimu Chuo Kikuu cha Dodoma Enos Magangali, ameishukuru Wizara kwa kushiriki katika mahafali hayo ya kuwaaga wahitimu wa Shahada ya Elimu na Maendeleo ya Jamii na kuomba ushirikiano zaidi katika kuwaandaa Wataalam hao muhimu katika jamii.

Jumla ya washiriki 521 walihudhuria wakiwemo wahitimu 381, wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili 120 pamoja na wageni waalikwa 20 walihudhuria sherehe ya mahafali hayo.