Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAKILI Peter Madeleka amejitosa rasmi kuwania Ubunge katika Jimbo jipya la Kivule,huku akiikosoa CCM Juu ya Hali Ngumu ya Maisha
Madeleka aliyejiunga na ACT Wazalendo hivi karibuni akitokea Chadema amechukua fomu Leo jijini Dar es Salaam.
Hafla ya kuchukua fomu hiyo imefanyika katika ofisi za chama hicho na kuhudhuriwa na umati wa wanachama pamoja na viongozi mbalimbali wa chama ngazi ya jimbo.

Fomu hiyo imekabidhiwa kwa Wakili Madeleka na Kaimu Katibu wa Jimbo la Kivule, Emmanuel Magoto.
Akizungumza baada ya kupokea fomu, Madeleka ameeleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Kivule kwa uadilifu na kuwahakikishia kwamba sauti zao zitasikika Bungeni.
Amegusia changamoto nyingi zinazolikabili jimbo hilo, zikiwemo miundombinu mibovu ya barabara ambazo hazipitiki kwa mwaka mzima na hivyo kusababisha usumbufu kwa wakazi na kudhoofisha shughuli za kiuchumi.
Pamoja na hayo, Madeleka ametumia jukwaa hilo kukosoa utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa umeshindwa kutatua matatizo ya msingi ya wananchi na kuendelea kusababisha hali ngumu ya maisha.
Aidha, amezungumzia hali ya kisiasa nchini na changamoto za demokrasia, akisisitiza kuwa licha ya mazingira magumu, ni muhimu kwa Watanzania kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kama njia ya kupigania mabadiliko.

“Hatuwezi kumsusia fisi bucha. Tunawajibu wa kupigania mabadiliko huku tukiendelea kushiriki. Kususa hakutatusaidia,” aliongeza.
Wakili Madeleka amesindikizwa na umati wa wanachama wa ACT Wazalendo na viongozi wa Jimbo la Kivule, hali iliyoashiria hamasa kubwa na matumaini miongoni mwa wananchi juu ya mustakabali mpya wa jimbo hilo.
