Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbinga

Wakulima wa zao la kahawa wanaohudumiwa na Chama cha msingi cha Ushirika Liyombo Amcos  Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma, katika msimu wa kilimo 2025/2026 wamezalisha kahawa  safi zaidi ya tani 1,674.9 sawa na kilo 1,674,925 yenye thamani ya Sh.bilioni 18,788,435,888.16.

Katibu wa Liyombo Amcos Angelina Nchimbi alisema, Sh.17,142,956,195.94 wamelipwa wakulima na fedha nyingine wamelipwa wadau wengine wanaojihusisha na tasnia ya kahawa wakiwemo wasafirishaji,ushuru wa Halmashauri na bodi ya Kahawa Tanzania.

Hayo yamesemwa na  Katibu wa Chama hicho Angelina Nchimbi,wakati akitoa taarifa za mapato na matumizi kwenye mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika katika ofisi za chama hicho kijiji cha Liyombo kata ya Linda.

Nchimbi alisema,katika msimu 2025/2026 chama kimekusanya  Sh.milioni 45,603,240 kati ya hizo Sh.milioni 43,754,780 zimetoka kwenye mradi wa gari na Sh.milioni 1,848,460 kutoka kwenye mradi wa shamba darasa.

Katibu wa Chama cha msingi cha ushirika Liyombo Amcos Angelina Nchimbi,akitoa taarifa ya maendeleo ya Chama hicho kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka.

Alisema,Chama kimetumia  Sh.34,135,000 ambapo Sh.26,300,000  zimetumika kukarabati nyumba ya walimu,Sh.7,835,000 kuanza ujenzi wa nyumba moja ya mwalimu ambayo imefikia hatua ya kupauwa.

Akizungumzia ukomo wa madeni ulioidhinishwa katika mkutano mkuu wa makisio wa mwezi Aprili 2025 alieleza kuwa,Chama kilikopa  Sh.450,000,000, Sh.100,000,000 zilitumika kununua mtambo  wa kukoboa kahawa na Sh.350,000,000 kununua pembejeo za wanachama.

“Tulipata mkopo wa Sh.100,000,000 ambazo zilitumika kwenye uendeshaji wa mtambo na kukusanya kahawa kilogram  307,070,pia katika awamu ya kwanza Ofisi ya Mrajisi iliidhinisha fedha Sh.300,000,000  kwa ajili ya kununua mbolea mifuko 4,828 UREA 1,690 CAN 2,103 na S.A mifuko1,035”alisema Nchimbi.

Aidha alisema,katika msimu 2024/2025 Chama hicho kilifanikiwa kukusanya kilo 980,829 za kahawa safi zilizowaingizia kiasi cha Sh.bilioni 10,965,241,344.4 na bei ya wastani kwa kilo moja ilikuwa Sh.8,126 na Chama kilipata Sh.85,056,920 kama ushuru.

Kwa mujibu wa Nchimbi,katika msimu 2026/2027 Chama kinatarajia kukusanya  kahawa tani 800 sawa na kilo 800,000 ambazo zitawaingizia Sh.milioni 80 kama ushuru,mradi wa gari Sh.milioni 65,mradi wa shamba darasa Sh.milioni 2 na Sh.milioni 1 kutoka  viingilio vya wanachama wapya.

Awali Mwenyekiti wa Chama hicho Joseph Mbele,amewataka wakulima kuwa waaminifu kwa kurudisha mikopo wanayochukua kutoka kwenye taasisi za fedha ili kuepuka kufikishwa kwenye vyombo vya sharia au kufilisiwa mali zao.

Mbele alisema,baadhi ya wakulima wa chama hicho sio waaminifu kwani wanakopa  fedha au pembejeo za kilimo kwa taasisi zaidi ya moja,hivyo kusababisha usumbufu  kwa chama ambacho  ndiyo mdhamini wa kwanza wa mkulima.

“Mkulima anakopa pembejeo kwenye taasisi za fedha  lakini hazitumiki kwa malengo,badala yake anakuja Amcos kuomba mkopo mwingine,naomba niwaambie kama viongozi hatutakuwa tayari kumsaidia mwananchi  huyo”alisema Mbele.

Mwenyekiti wa Liyombo Amcos Joseph Mbele,akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho uliofanyika jana. 

Kwa upande wake Afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya Mbinga Leo Kumburu,amepiga marufuku vyama vya msingi vya ushirika”Amcos) katika Halmashauri hiyo kutopokea kahawa mbichi zinazoletwa na wakulima.

Kumburu,amewataka wakulima kuanza maandalizi ya kupata pembejeo mapema na wahakikishe wanapeleka kahawa wanazovuna kwenye vyama vya ushirika  vyenye dhamana ya kuuza na kusimamia soko la kahawa ili kupata bei nzuri badala ya kuuza kwa njia za magendo.