Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbinga
Wakulima Mkoani Ruvuma,wametakiwa kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na wataalamu ili waweze kupata mazao mengi na bora na kupata soko la uhakika, badala ya kutumia mbegu zinazouzwa mitaani.
Wito huo umetolewa na Mtafiti kutoka kituo cha Utafiti Tanzania(TARI) Naliendele Mkoani Mtwara Stella Andrew,wakati akizungumza na Wakulima katika Kijiji cha Amanimakolo Wilayani Mbinga.
Andrew amesema,baadhi ya wakulima hapa nchini,wanapata hasara kwa kuwa wanatumia mbegu zisizofanyiwa utafiti ambazo haziendani na mazingira halisi ya kilimo kwenye maeneo husika.
Aliwahakikishia wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kuwa,mbegu zote zinazozalishwa na kufanyiwa utafiti na TARI ni bora,zinazingatia usalama na zimeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima kwenye maeneo mengi hapa nchini.

Amesema kuwa,Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi hapa nchini, lakini tija ni ndogo kutokana na baadhi ya wakulima kutumia mbegu za kienyeji ambazo hazijafanyiwa utafiti.
Aidha amesema,TARI ina jumla ya vituo 17 vya utafiti wa zao la korosho katika maeneo mbalimbali vilivyoanzishwa ili kutoa elimu juu ya zao la korosho kwa ajili kuwaondolea wakulima usumbufu kwenda mbali na maeneo yao kupata elimu ya zao hilo.
Amesema,katika Mkoa wa Ruvuma kuna vituo vitano vya uendelezaji wa zao la korosho vilivyopo katika kijiji cha Nandembo na Chikomo Wilaya ya Tunduru,Paradiso Wilaya ya Mbinga na Lusewa Wilaya ya Namtumbo.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa TARI Bezetina Kiswaga amesema, wamekuja na teknolojia mbili ikiwemo matumizi ya mbegu bora za karanga na ufuta.
Amesema,wanazo mbegu mbalimbali za karanga zinawafaa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma na faida ya mbegu hizo hazishambuliwi na magonjwa kama mbegu nyingine za kienyeji na hazishambuliwi kirahisi na wadudu na zinastahimili ukame.
“Mbegu hizi zimesheheni madini mbalimbali kama vile madini ya protin,madini ya Kashiam na zinki ambayo yanasaidia kuboresha afya ya mwili na zinatoa mavuno mengi kuanzia tani 1.5 kwa hekta moja,tunawashauri wakulima wa Mkoa wa Ruvuma watumie mbegu bora kutoka kituo cha utafiti Naliendele”amesema Kiswaga.
Kwa upande wa mbegu za ufuta Kiswaga amesema,wanazo aina nne ambazo ni Lindi 2002,Ziada,Mtondo na Mtwara ambazo zinakomaa mapema,hazishambuliwi na magonjwa na zinastahimili magonjwa mbalimbali kulingana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Naye Mtafiti wa mazao ya nafaka Juma Mfaume amesema,katika maenesho ya mwaka huu wameleta mbegu aina mbalimbali za nafaka ikiwemo mbegu bora ya mtama,mbegu ya ulezi na njungu mawe.
Amesema,lengo la kuleta mbegu hizo ni kwa sababu wakulima wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini hususani Mkoa wa Ruvuma wanajihusisha na kilimo cha nafaka na mikunde.