Na Mwandishi Wetu, JahuriMedia, Mbinga
Wakulima wa zao la kahawa kijiji cha Liyombo kata ya Linda Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma,wametakiwa kujenga mazoea ya kupanga bajeti ya fedha mara wanapouza mazao ikiwemo kahawa kwa kuimarisha chama chao,kufanyia shughuli za maendeleo na kuanzisha biashara ili kujiongezea mitaji.
Wito huo umetolewa na Afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya Mbinga Leo Kumburu,wakati akizungumza na wakulima wa kahawa wanaohudumiwa na Chama cha msingi cha Ushirika Liyombo Amcos kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama hicho.
Kumburu alisema,wakulima wanatakiwa kutunza fedha wanazopata kupitia shughuli za kilimo badala ya kuzifuja kwa kufanya matumizi yasiyo ya lazima yakiwemo kunywea pombe na wanaume kuongeza mke,hivyo kujikuta katika lindi la umaskini licha ya kupokea fedha nyingi zinazotokana na mauzo ya mazao wanayozalisha.
Alisema,mkulima akijiwekea akiba itamwezesha kujiepusha na mikopo kutoka katika taasisi za fedha au mikopo ya kausha damu kwa kukopa fedha kwa kwa watu wasio rasmi ambao hutoa fedha kidogo na kuwadai mazao mengi yasiolingana na fedha walizokopeshwa.
Aidha,amezitaka taasisi za fedha kwenda moja kwa moja kwa wakulima vijijini ili kutoa elimu kuhusu umuhimu kwa kuwa na akaunti kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya kahawa, badala ya malipo yao kupitishwa kwenye akaunti za watu wengine.
Mkulima wa kahawa wa kijiji hicho Badwin Ndunguru,ameshauri viongozi wa Chama hicho kununua mtambo mpya ambao utasaidia wakulima kupata kahawa safi baada ya kukoboa kabla ya kupeleka kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
“mtambo mpya utatusaidia sana sisi wakulima kupata kahawa safi na bei nzuri kwenye soko la ndani na nje,hivyo nashauri viongozi wetu anzeni mchakato wa kupata mtambo mpya ambao utatusaidia wakulima kupata kahawa safi ambao utatuhamasisha kuongeza uzalishaji wa kahawa mashambani badala ya kutumia mtambo wa zamani”alisema.
Mwakilishi wa kiwanda cha kahawa Mbinga(MCCCO)Keneth Ndunguru,amewapongeza wakulima wa kijiji hicho kwa kuzalisha kahawa kwa wingi na safi iliyopokwa katika kiwanda hicho kwa ajili ya kukobolewa.
Ndunguru,amewasisitiza wakulima kupitia Chama cha msingi Liyombo Amcos kuendelea kushirikiana na MCCCO kwa kupeleka kahawa kwani kina mtambo mkubwa na wenye uwezo wa kukoboa kahawa kwa haraka na kinamilikiwa na wakulima wenyewe kwa zaidi ya asilimia 64 tofauti na viwanda vya watu binafsi.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wa Kahawa wilaya ya Mbinga(Mbifacu) Erick Kinunda,amewapongeza wakulima wanaohudumiwa na Liyombo Amcos kwa kazi kubwa ya kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa misimu mitatu mfululizo.



