NIRC – Geita
Zaidi ya wananchi 747 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa uchimbaji visima vya Umwagiliaji 36 unaotekelezwa katika kijiji cha Mwilima Mkoani Geita, ambapo visima hivyo vitamwagilia zaidi ya ekari 1440 katika vijiji 32, lengo ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa mazao na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uchimbaji wa visima Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.Martin Shigela, amesema kuwa utekelzaji wa mradi huo utachangia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza ajira, kuongeza thamani ya mazao, na kurahisisha upatikanaji wa chakula na mazao ya biashara kwa wananchi wa kijiji cha Mwilima.

Aidha, Mhe. Shigela ametumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha usalama wa vifaa na mitambo ya umwagiliaji,unakuwa wa kutosha kwakila mmoja kushiriki katika ulinzi wa rasilimali hizo ili kuhakikisha mradi unadumu kwa muda mrefu.
Aidha Mhandisi Umwagiliaji Mkoa wa Geita Boniface Mkita amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali kupitia Tume inaendelea na utekelezaji wa kazi ya uchimbaji wa visima kwa kutumia mitambo ya Serikali.
Pia ameongeza kuwa kwa awamu ya kwanza, visima 36 vitachimbwa katika vijiji 32 Mkoani humo, ambapo ekari 1,440 zitamwagiliwa na kuhudumia wakulima zaidi ya 747.

Utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa ushirikiano kati ya Tume na halmashauri husika, na unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili (2). Kati ya visima hivyo, visima 30 tayari vimefanyiwa uhakiki wa awali.
Mhandisi Mkita amesema kuwa kilimo cha Umwagiliaji kitawawezesha wakulima kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa mazao, pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao yenye thamani kubwa yatakayowapatia wakulima kipato kikubwa kutoka eneo dogo.
Miongoni mwa kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na utafiti na upimaji wa maeneo ya uchimbaji, uchimbaji wa visima vyenye urefu usiozidi mita 250, uwekaji wa mabomba yenye kipenyo cha inchi 6 hadi 8, pamoja na ufungaji wa mifumo ya kusukuma maji kwa kutumia pampu.

Sambamba na hayo ,kutajengwa minara ya kuwekea tenki za maji, kununuliwa na kufungwa matanki yenye ujazo wa lita 10,000, pamoja na mabomba ya inchi 3 yatakayofikisha maji shambani.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwilima akiwemo Ndagaile Lusanda na Stephano Malehe wameishukuru serikali kwani visima hivyo vitasaidia kuinua vipato vyao kwa kulima mazao ya mbogamboga pamoja na mazao mengine.



