Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaha
Wanafunzi 2,328 kutoka Shule ya Msingi Mailimoja na Sekondari ya Bundikani zilizopo Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani wamefanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo.
Upimaji huo umefanyika katika kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema watoto sita wamepatiwa rufaa kufika JKCI kwaajili ya uchunguzi zaidi na watoto wawili wamepewa rufaa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi).
Dkt. Stella alisema baada ya wanafunzi hao kufanyiwa kipimo cha kuangalia mapigo yao ya moyo wanafunzi 34 waliokuwa na viashiria vya magonjwa ya moyo walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) ambapo watoto sita walikutwa na magonjwa ya moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi waliofanyiwa upimaji huo wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwafikia na kuwapa elimu kuhusu magonjwa ya moyo.
Shania Hassan wa shule ya Sekondari Bundikani alisema hapo awali hakuwa na elimu kuhusu magonjwa ya moyo lakini kupitia kambi hiyo ameweza kupata elimu ambayo itamsaidia kujikinga na magonjwa hayo.
“Tumesisitizwa kufanya mazoezi kwa afya, leo nimepata nafasi ya kujua umuhimu wa kufanya mazoezi, lakini pia nimejua mazoezi ni sehemu ya kinga dhidi ya magonjwa ya moyo”, alisema Shania.
Naye Emmanuel Mangano aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafuata na kuwapa huduma hivyo kuiombea Taasisi hiyo iendelee kufanikiwa zaidi katika kutoa huduma za matibabu ya moyo.
“Leo nimefurahi sana nimepata elimu nzuri kuhusu magonjwa ya moyo, Taasisi hii inavyoendelea kutoa huduma za upasuaji wa moyo iendelee kufanikiwa na kujulikana zaidi”. Alisema Emmanuel.

