Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungìano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa wanahabari wa Afrika kuandika habari chanya zinazolijenga Bara la Afrika badala ya kutegemea simulizi hasi kutoka vyombo vya nje.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika uliofanyika AICC jijini Arusha, Dkt. Mpango amesema Afrika ina uwezo mkubwa uthabiti na maendeleo yanayopaswa kuangaziwa zaidi.

Ametoa mfano wa vijana wavumbuzi, wanawake jasiri na mchango wa bara hilo katika sayansi na uchumi wa dunia, hivyo kuhimiza vyombo vya habari kutumika kama daraja la mawasiliano, uhifadhi wa historia na urithi wa Afrika sambamba na kuendeleza Ajenda ya AU 2063.

Dkt. Mpango pia amehimiza mabaraza ya habari kuandaa mapendekezo ya kisera na kisheria yatakayoongoza matumizi bora ya akili unde (AI) kwa kuzingatia maadili ya taaluma.

“Ila nitahadharishe kuhusu changamoto ya taarifa potofu zinazotolewa kimakusudi na nisisitize umuhimu wa mifumo bora ya sheria kudhibiti hali hiyo, vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika ukuaji wa uchumi kupitia utoaji wa taarifa sahihi kuhusu ajira, mitaji, na huduma za kifedha”

Pia amesisitiza kuwa vyombo hivyo viwe na sera jumuishi hasa kwa watu wenye mahitaji maalum.

Makamu wa Rais ameyataka mabaraza ya habari kuwa imara katika kulinda uhuru wa kujieleza na kushughulikia kwa ufanisi malalamiko dhidi ya vyombo vya habari na kushauri kuimarishwa kwa uwezo wa wanahabari kupitia mafunzo ya kitaaluma ili kukabiliana na taarifa potofu.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi ametoa shukrani kwa tuzo iliyotolewa kwa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa mchango wake katika kuanzisha vyombo binafsi vya habari.

Amesema vyombo hivyo ni njia muhimu ya kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

Akipokea Tuzo ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania kwa niaba ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere amesema vyombo vya habari ni nguzo ya uhuru wa mawazo.

Ameeleza kuwa katika harakati za ukombozi vyombo hivyo vilitumika kueneza ujumbe wa haki na utu wa Mwafrika.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika Ernest Sungura, amesema changamoto za tasnia ya habari Afrika zinahitaji ushirikiano wa pamoja na kwamba uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu katika kufichua maovu na kuelimisha jamii.

Mwakilishi wa vyombo vya habari binafsi Rostam Aziz ameonya kuhusu mijadala inayoendeshwa na watu waliopo nje ya nchi wasiowajibika kwa maudhui yao.

Ametoa wito kwa sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya habari ili kukuza uhuru wa fikra na maudhui ya kitaifa.

Kauli mbiu ya mkutano ilikuwa: “Uboreshaji wa Sheria za Vyombo vya Habari na Mawasiliano ni Msingi wa Weledi wa u
Uandishi wa Habari.”