Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Jumla ya wananchi 1,300 kutoka kata za Mbwawa na Visiga wamejitokeza na kunufaika na huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), hususan upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa, ndani ya siku tatu za ziara ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, Mwajuma Nyamka.
Kati ya wananchi hao, 850 walitoka katika kata ya Visiga huku wengine wakitoka kata ya Mbwawa, wakichangamkia fursa hiyo ambayo imewarahisishia kupata huduma zilizokuwa zikihitaji kusafiri umbali mrefu na kutumia muda zaidi.
Akizungumza Aprili 11, 2026 katika kata ya Misugusugu, Nyamka alieleza huduma hizo za karibu zimeondoa changamoto ya umbali na ucheleweshaji wa upatikanaji wa vyeti hivyo muhimu.
Alifafanua tayari vyeti vilivyokamilika vimekabidhiwa kwa Mwenyekiti wa CCM wa kata ya Visiga ili kuhakikisha vinawafikia walengwa kwa wakati.
Vilevile, Nyamka aliwataka mabalozi wa CCM kuendelea kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na chama kwa kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi na kuziwasilisha kwa mamlaka husika, sambamba na kueleza mafanikio yanayotekelezwa na Serikali.
Msajili Mwandamizi wa RITA Wilaya ya Kibaha, George Chuwa, alieleza wananchi wote 1,300 waliowasilisha nyaraka na kulipa ada ya shilingi 20,000 wamekamilishiwa vyeti vyao.
Kwa mujibu wa Chuwa, majina yaliingizwa kwenye mfumo na kuchakatwa kwa haraka, ambapo vyeti vilikamilika ndani ya saa 48, huku akitaja changamoto ya baadhi ya wananchi kushindwa kumudu gharama za malipo kwa wakati.
Aliwataka wananchi kufuata taratibu sahihi za kupata vyeti hivyo na kuepuka vitendo vya kughushi nyaraka au kupata vyeti kwa njia zisizo halali, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Naye Katibu wa UWT Kibaha Mjini, Cecilia Ndalu, aliwahamasisha wanawake kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, huku akisisitiza umuhimu wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa wengine kunufaika.
Diwani kata ya Misugusugu Ally Simba alieleza kuna changamoto ya kuharibika kwa barabara baada ya mvua zilizonyesha, wanatarajia kuzifanyia matengenezo baada ya msimu wa mvua kukata maana mitaa ilishatoa taarifa ya barabara zenye changamoto na wanakabiliana na kero hiyo.





