Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kwimb
Wananchi Wilayani Kwimba na maeneo jirani, wameishukuru Taasisi ya Doris Mollel (Doris Mollel Foundation) kwa kuleta mabadiliko makubwa katika wilaya hiyo, baada ya kufadhili na kusimamia ujenzi wa jengo la kisasa la Kimataifa la kuwahudumia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, jengo linalosogeza huduma hizi muhimu karibu na wananchi kwa mara ya kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Doris Mollel , akieleza kuwa jengo hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya Watoto.

Mkazi wa Kwimba, Joyce Emmanuel James, ameishukuru Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kujenga jengo hilo, akieleza changamoto walizokuwa wanapitia kabla ya uwepo wa huduma hizo karibu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Alex Ntale Gasasira, ametambua uwekezaji huo na kusisitiza umuhimu wa uwepo wa huduma hizi karibu na jamii, akieleza kuwa mfumo huo unaendana na miongozo ya WHO inayosisitiza umuhimu wa Mama na Mtoto kuwa pamoja wakati wa matibabu.
Jengo hilo la kimataifa linalotarajiwa kuzinduliwa tarehe 28 Februari 2026 ,limefadhiliwa na kujengwa na Taasisi ya Doris Mollel (DMF) kwa lengo la kuboresha huduma za Watoto wachanga na kuleta matumaini mapya kwa Familia za Kwimba na maeneo ya jirani na limegharimu takribani Bil. 2.125 kwa kushirikiana na Taasisi ya Keep A Child Alive na Jhpiego.








