Na Mary Margwe, JamhuriMedia, Manyara

Mbio za Mwenge wa Uhuru hufanyika kila mwaka na kukimbizwa nchi nzima ikiashiria kuangaza nchi na kuvuka mipaka kuleta matumaini palipo kukata tamaa, upendo palipo uadui na heshima palipo chuki.

Mwenge wa Uhuru hapa nchini ulinyanyuliwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro mnamo Desemba 9, 1961 na shujaa Brigedia Alexander Nyirenda.

Sababu ya huyu brigedia Nyirenda kunyanyua mwenge huu ni kuonesha fahari ya nchi na pia kuleta matumaini kwa Watanzania wote kwa kutokata tamaa, kupendana, kuheshimiana na kutogombana ikimaanisha kuwa na ushirikiano.

Mwenge wa Uhuru unapokimbiza unakua na kazi kuu ya kukagua miradi, kuweka mawe ya msingi katika miradi, kufungua, kuzindua miradi mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga Julai 12, 2025 anapokea Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha Mbuguni Wilaya ya Meru, Mkoani Arusha anapokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Laban Kihongosi.

Sendiga anasema Mwenge wa Uhuru ni moja ya alama muhimu ya umoja wa Nchi yetu na utaifa wetu kwa kuzingatia hilo, Wananchi wa Mkoa wa Manyara wanatambua falsafa za Mwenge wa Uhuru kuwa ni chachu ya kuleta maendeleo endelevu, kuleta matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.

Anasema wananchi wote wa Mkoa wa Manyara tuko bega kwa bega nanyi katika kuendeleza azma hii kwa lengo la kujiletea maendeleo endelevu ya Mkoa wetu, ambapo anaongeza haya mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ali Ussi.

Aidha Mkuu huyu wa Mkoa wa Manyara Sendiga anafafanua kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zinatukumbusha mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) kwa kuiletea Tanzania Heshima, Upendo, Mshikamano, Amani, Umoja na Utulivu. Maono yake bado yanasimama, yanaheshimika na yanaendelea kuwa dira na kichocheo cha kuendeleza Mbio hizi za mwenge.

“Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ali Ussi, Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Manyara, utakimbizwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa saba (7) ambazo ni Simanjiro, Kiteto, Babati Wilaya, Babati Mji, Mbulu Mji, Mbulu Wilaya, na Hanang kwa mzunguko wa kilometa 1,197.10.” anasema Sendiga.

” Mwenge wetu wa Uhuru ukiwa Mkoani Manyara utatembelea miradi 51 yenye thamani ya sh. bil. 71.3 kwa kufanya kazi zifuatazo, kuweka mawe ya msingi miradi 11 yenye thamani ya sh. Bil. 9.7, Kuzindua miradi 16 yenye thamani ya shil. bil. 5.5, Kufungua mradi 1 wenye thamani ya sh. Mil. 98.4; na Kukagua/kuona miradi 23 yenye thamani ya shilingi bilioni 55.9″ anafafanua Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga.

Akielezea hali ya uchangiaji wa mchango katika miradi hii Sendiga anafafanua kuwa nguvu za Wananchi sh. Mil.330,
Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mapato ya Ndani) Bil. 1.9, Serikali Kuu sh. Bil.62.2, Wadau wengine ni sh.Bil.6.9nhuku ikileta jumla kuu ni sh. Bil. 71.3

” Nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Manyara kwa kuiibua, kuianzisha, kuchangia na kuitekeleza miradi hii na , kipekee niwashukuru wananchi na wadau wa maendeleo ambao wameweza kuchangia shughuli za maendeleo katika Mkoa wetu” anasema Sendiga.

” Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Pamoja na Jumbe nyingine za kudumu za Mwenge wa Uhuru, Mkoa wa Manyara tumejiandaa kupokea ujumbe Mahsusi ambao ndio Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 isemayo Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa Amani na Utulivu inalenga kuhamasisha ushiriki mpana wa wananchi katika mchakato wa kuwachagua viongozi wao kwa nafasi za Rais, Wabunge na Madiwani kupitia uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025 huku tukidumisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi yetu” anafafanua Mkuu wa Mkoa huyo.

Sendiga anaongeza kuwa Mkoa wa Manyara umejipanga kuitekeleza kauli mbiu hii kwa kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama, na wadau mbalimbali kwa kuhakikisha, Wananchi wote wenye sifa wanashiriki uchaguzi kwa uhuru na amani, Wagombea wanafanya kampeni kwa kufuata sheria, kanuni na ratiba zitakazotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambapo vyama vyote vinashiriki bila bughudha, na
uchaguzi unafanyika kwa mazingira ya utulivu.

” Tunaamini kuwa utekelezaji wa kaulimbiu hii utaleta hamasa kubwa na ya kizalendo kwa wananchi wa mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali kwa njia ya kidemokrasia na si vinginevyo ” anaongeza Sendiga.