Miaka ya adha yafikia kikomo, usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii sasa warahisishwa
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ngorongoro
Wananchi wa Kata ya Oldonyosambu, wilayani Ngorongoro, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja la mawe lenye urefu wa mita 45 katika Mto Mbaga linalounganisha vijiji vya Jema na Oldonyosambu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kukamilika kwa daraja hilo kumewaondolea changamoto ya muda mrefu ya usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma za kijamii hususan katika kipindi cha masika.
Diwani wa Kata ya Oldonyosambu, Mhe. Kabaney Mojah, amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo, wakazi wa eneo hilo walikumbwa na matatizo makubwa ya mawasiliano na usafirishaji wa mazao kutoka Kijiji cha Jema ambako kuna shughuli za kilimo.
“Kijiji cha Jema ni eneo letu kuu la uzalishaji mazao. Hapo awali tulikuwa na changamoto kubwa ya kusafirisha mazao kwenda soko la Arusha pamoja na mawasiliano kati ya vijiji hivi viwili. Tunaishukuru Serikali kwa kutatua tatizo hili,” alisema Mhe. Mojah.
Aliongeza kuwa Mto Mbaga ulikuwa kikwazo kikubwa, hasa nyakati za mvua, hali iliyosababisha usumbufu hata katika masuala ya dharura.
“Mto Mbaga ni mto korofi, zamani wakati wa masika wananchi hawakuweza kuvuka kabisa. Sasa tunaweza hata kuwasafirisha wanafunzi wanaougua kutoka Shule ya Sekondari Jema hadi Hospitali ya Wilaya iliyopo Wasso bila hofu,” amesisitiza.
Naye, mkazi wa eneo hilo Bw. Likam Maroseck amesema kabla ya daraja kujengwa, baadhi ya wananchi walikumbwa na hatari ya kusombwa na maji walipokuwa wakivuka kwenda kulima mashamba yao kijijini Jema.
“Ujenzi wa daraja hili umeleta ahueni kubwa. Kwa sasa shughuli zetu zinafanyika kwa urahisi na usalama zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Ngorongoro, Mhandisi Edwin Merdad, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, walitenga bajeti ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo pamoja na uboreshaji wa barabara inayounganisha vijiji hivyo.
Amesema pamoja na mpango wa awali wa kuchonga na kuweka kifusi kwenye barabara yenye urefu wa kilomita tano, wamefanikiwa kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 14 kati ya vijiji hivyo viwili.
“Daraja hili ni msaada mkubwa si tu kwa wakazi wa Oldonyosambu na Jema, bali pia kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani ya Kenya wanaoshiriki katika shughuli za minada.
“Zamani wakati wa masika wananchi walishindwa kuvuka kwa takribani miezi miwili, lakini sasa hali hiyo imekuwa historia,” amesema Mhandisi Merdad.
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ina mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 970.698, zikiwemo barabara za zege kilomita 0.224, barabara za changarawe kilomita 306.41 na barabara za udongo kilomita 664.064.








