Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imeendelea kutoa huduma za Ushauri na Elimu ya masuala mbalimbali ya Kisheria katika Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Manyara, Kliniki hiyo inafanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Manyara.

Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara ilianza tarehe 19 na inatarajia kukamilika tarehe 25 Januari, 2026 katika viwanja vya Mount Hanang, Kateshi Mkoani Manyara.

Akizungumzia kuhusu Kliniki hiyo, Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Neema Ringo amesema wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za Ushauri wa Kisheria katika Kliniki hiyo ambapo wengi wao walikuwa na changamoto katika maeneo ya migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa, ajira na mirathi.

“Kliniki hii imekuwa na mafanikio makubwa kwani wananchi wengi wamejitokeza na mawakili wetu wameweza kuzitatua kero za wananchi hao, masuala ya ardhi, ajira, ndoa na mirathi yalijitokeza zaidi.”

Aidha, Bi. Neema Ringo amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikiwa kutatua baadhi ya migogoro hapohapo wakati wa Kliniki na baadhi ya changamoto za kisheria zimechukuliwa kwa ajili ya hatua zaidi ya kuzitatua.

“Tumeweza kutatua changamoto za wananchi hapahapa kuna baadhi ya wananchi wamekuja na changamoto zao za Kisheria tumezifanyia kazi na kuzimaliza, baadhi ya changamoto tunaendelea nazo kwa ajili ya hatua zaidi za utatuzi.” Alisema Bi. Ringo.

Vilevile, Bi. Neema Ringo aliwashukuru Mawakili wote waliotoa huduma katika kliniki ya Sheria Manyara.

“Binafsi nawashukuru na kuwapongeza Mawakili wote walioshiriki katika zoezi hili la kutoa huduma kwa Wananchi ambao hawana uwezo wa kulipia huduma ya Sheria, hii ni Sadaka, nawashukuru sana kwa Huduma hii.” Alisema Bi. Neema Ringo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa , Bw. Lameck Buntuntu ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu zoezi la kuzindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria katika Mkoa wa Manyara pamoja na kuendesha Kliniki hiyo kwa kuwashirikisha Mawakili na Wanasheria kutoka kwenye Taasisi nyingine za Serikali.

Tunaipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuichagua Manyara kuja kuzindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria, sisi tunawaahidi kuendelea kutoa huduma hizi za kisheria kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao.” Amesema Bw. Buntuntu

Kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Manyara Bi. Cecilia Sulle ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikiana na Mkuu wa Mkoa kwa kuletewa huduma ya Kliniki ya Sheria bila Malipo.

“Nashukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Mkoa kwa huduma hii, sisi wajane na watu wa hali ya chini tumekuwa tukikosa haki zetu, lakini kwa kliniki hii nimeweza kupata msaada na kupata haki yangu.” Alisema Bi. Cecilia

Kliniki ya Sheria bila Malipo Mkoa wa Manyara ilianza tarehe 19 Januari, 2026 na itakamilika tarehe 25 Januari, 2026 katika Viwanja vya Mount Hanang Katesh.