Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema jumla ya wananchi 13,550 wamejitokeza kupata huduma mbalimbali za sekta ya ardhi kupitia Samia Ardhi Kliniki iliyofanyika katika mikoa yote 26 nchini.
Dkt. Akwilapo amesema hayo wakati akifunga rasmi Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026, akisema kliniki hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi hususan wanawake.
Amesema, kati ya wananchi waliojitokeza katika kliniki hizo, wanawake walikuwa 8,725 sawa na asilimia 64.4 huku wanaume wakiwa 3,892 sawa na asilimia 35.7, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wanawake katika kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.
Aidha, Waziri Akwilapo amesema, jumla ya hatimiliki 3,131 zimetolewa kwa wananchi waliokamilisha taratibu za umilikishwaji wa ardhi ambapo hatimiliki 2,081 sawa na asilimia 57.4 zimetolewa kwa wanawake na hatimiliki 1,543 sawa na asilimia 43.6 zimetolewa kwa wanaume.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo imeongeza usalama wa milki kwa wananchi pamoja na kuimarisha uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.
“Ardhi ni msingi wa uchumi wa mwananchi na Taifa. Mwanamke anapomiliki ardhi kisheria anapata uwezo mkubwa wa kuwekeza, kufanya shughuli za uzalishaji na hata kupata mikopo katika taasisi za fedha,” alisema.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi amesema, Samia Ardhi Kliniki imenufaisha wanawake kwa kuwaelimisha jambo alilolieza kuwa limelenga kuwawezesha na kulinda haki na kutatua changamoto zao.
‘’Kupitia Kliniki hiyo wanawake walipewa huduma mbalimbali ambazo ni elimu ya kumiliki ardhi, ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya ardhi pamoja na utoaji hati’’ amesema Kanali Msengi.







