Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, halmashauri 180, kata 1,907 na vijiji/mitaa 5,702 vimefikiwa, ambapo wananchi wapatao 2,698,908 walinufaika kwa kupata elimu na huduma za kisheria.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ameeleza hayo Mei 20, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, akieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya sheria na haki chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, ameeleza kuwa idadi ya mashirika yanayotoa msaada wa kisheria imeongezeka kutoka 84 mwaka 2021 hadi 377 mwaka 2025, huku wasaidizi wa msaada huo wakiongezeka kutoka 617 hadi 2,205.

Pamoja na hayo, amesema Serikali imeanzisha Madawati ya Msaada wa Kisheria katika mamlaka 184 za serikali za mitaa na kuwaajiri watumishi 449 ili kuyasimamia. Tangu kuanzishwa kwa madawati hayo, wananchi 6,427,738 wamepatiwa elimu ya sheria na haki za binadamu.

Katika hatua ya kuimarisha utawala wa sheria, Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekamilisha uhakiki wa Sheria Kuu 300 kati ya 446 zilizotafsiriwa kwa Kiswahili, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote.

Waziri Ndumbaro pia alitangaza uwepo wa Kituo cha Huduma kwa Mteja kinachorahisisha upokeaji wa malalamiko kupitia simu, WhatsApp na barua pepe.

Amesema kati ya mwaka 2021 hadi 2025, idadi ya majaji imeongezeka kutoka 92 hadi 146 na mahakimu kutoka 1,412 hadi 1,426. Hali hiyo imesaidia kupunguza mrundikano wa mashauri ambapo mashauri ya muda mrefu ni asilimia 4 tu ya yaliyosalia mahakamani.

Serikali pia imekamilisha ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika mikoa sita na inaendelea na ujenzi wa vituo tisa zaidi. Mahakama za Wilaya na za Mwanzo zimejengwa na kukarabatiwa kwa kasi ili kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Vilevile, matumizi ya TEHAMA katika sekta ya sheria yameongezeka kwa asilimia 75, huku mifumo ya HAKI SHERIA na ya kutafsiri hukumu kwa Kiswahili na Kiingereza ikiimarishwa ili kurahisisha upatikanaji wa kumbukumbu za kimahakama.

Ofisi za Mashtaka zimeongezeka kutoka 53 mwaka 2021 hadi 108 mwaka 2025, huku watoa huduma 498 wakisajiliwa kwa ajili ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.

Katika eneo la usajili wa watoto, zaidi ya watoto milioni 10 wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa tangu mwaka 2021, hatua iliyoifanya Tanzania kutambuliwa kwa daraja “A” na taasisi ya kimataifa ya haki za binadamu kutokana na juhudi zake katika utawala bora.

Kwa upande wa elimu ya sheria, jumla ya wanafunzi 5,333 wamesajiliwa na 2,375 kuhitimu mafunzo ya uanasheria kwa vitendo tangu 2021. Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimehitimisha wanafunzi 2,876 katika ngazi ya cheti na astashahada.

“Mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha haki inatolewa kwa wote kwa haraka, kwa usawa na kwa gharama nafuu,” alisisitiza Dkt. Ndumbaro huku akiwasihi wananchi kutumia huduma za kisheria zinazotolewa na serikali.