*Asisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi ,utawala bora
*Aishangaa CHADEMA kuwa na kauli mbiu ya No Reform No election kuzuia uchaguzi
*Atuma ujumbe kwa wana CCM kutenda haki kupata wagombea ubunge udiwani
Na Mwandishi Wetu, Ukerewe
MAKAMU Mwenyekiti wa ChamaCha Mapinduzi (CCM) Bara Stephen Wasira, amesema utawala bora ni kutii Katiba na Sheria za nchi, hivyo mtu yeyote asiyetii na anataka kufanikisha mambo yake binafsi kwa kuua watu anakuwa sawa na gaidi.
Akizungumza jana katika kikao cha ndani na wanachama wa Chama hicho Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza , Wasira alitumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa wananchi kufuata Katiba na Sheria katika kufanya shughuli mbalimbali badala ya kuvunja sheria kwa kisingizio cha uhuru wa demokrasia.
Wakati akieleza hayo Wasira alionesha kukishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)ambacho kimekuwa na kauli mbiu yake ya ‘No Reform No Election’ yenye lengo la kuvuruga uchaguzi mkuu mwaka huu na kuhoji kama hawataki kupiga kura kwanini walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
“Asiyetii Katiba na sheria maana yake anataka nchi isitawalike, watu wapigane wenyewe kwa wenyewe, halafu wewe eti haki yako unaitaka katika mazingira ya mauaji bila kujali matokea yake, hilo haliwezekani”.

Wasira alifafanua kwamba kwa akili ya kawaida unaweza kujiuliza Katiba ipo inasema kila baada ya miaka mitano unafanyika Uchaguzi Mkuu halafu anatokea mtu anasema hakuna uchaguzi.
“Anasema hivyo kwa kutumia Katiba ipi? Katiba inaeleza wazi huwezi kughairisha uchaguzi alafu wewe unasema lazima usiwepo,kutaka kuzuia uchaguzi ni kinyume na Katiba na ni kutaka kuanzisha fujo…
“Je huo ndio utawala bora? Katiba inasema kila baada ya miaka mitano tunafanya uchaguzi wewe unasema hautafanyika…utawala bora ni kutii katiba na sheria na sio kutaka kukamilisha mambo binafsi kwa kukiuka sheria za nchi.”
Wasira alisema sababu inayoweza kufanya uchaguzi usifanyike ni vita na katika nchi yetu hakuna vita,hivyo hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi na kuwahakikishia wananchi kuwa uchaguzi mkuu uko pale pale na tayari uchaguzi ulishaanza kwa wananchi kujiandikisha katika daftari la kupiga kura.
Pia alisema kauli mbiu ya ‘No Reform No Election’ inaenda kufa muda si mrefu kwasababu tayari imezidiwa nguvu na Oktoba Tunatiki, na ushahidi wa hilo Watanzania wako tayari kwenda kupiga kura kwani wamejiandikisha.

“Tumewajibu wapinzani kwa kuja na kaulimbiu ya Oktoba Tunatiki, ambayo imeanzishwa na vijana na wapigakura wa chama,”alisema Wasira ni kuwasisitiza wana CCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa na mshikamano.
“CCM iko imara na kimejiandaa vya kutosha kushinda uchaguzi kwakuwa wamefanya mambo mengi ya kimaendeleo yanayoonekana ambayo wananchi wameyakubali.”
ATUMA UJUMBE KWA
WAPIGAKURA CCM
Katika hatua nyingine zikiwa zimebakia siku tano kuanzia leo Bunge Kuvunjwa,Makamu Mwenyekiti Wasira ametuma ujumbe mzito kwa wanachama wa Chama watakaoshiriki vikao kupata wagombea ubunge na udiwani kuhakikisha wanatenda haki na kupendekeza wagombea wanaokubalika kwa wananchi.
Akizungumza na wana CCM hao , Wasira alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa mchakato wa kupata wagombea udiwani na ubunge kuwa haki na kwamba tayari CCM wanaye mgombea urais wao Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dk. Emmanuel Nchimbi.
“Sasa kazi iko kwa wabunge na madiwani. Juni 28 mwaka huu Bunge linavunjwa…hivyo wabunge watakuwa wamebakisha siku tano wakati madiwani wao tayari wako likizo.Kwa sasa tumeongeza idadi ya wapiga kura na tutakuwa na wagombea watatu ambao watapigiwa kura za maoni kupitia vikao vya wana CCM.
“Utaratibu uliopo hivi sasa kutakuwa na vikao vya kata kwa madiwani na vikao vya wilaya kwa wabunge, ndio vitaanza kutupa maoni yao kwa wale watakaochukua fomu Juni 28.Wapiga kura wasikilizeni wananchi wanamtaka nani kugombea ubunge au udiwani.”
“Jambo la pili katika kupendekeza wagombea tendeni haki kwenye vikao, kuna hadithi ya mama mmoja, mumuwe alikuwa anagombea mtaa akaambulia kura sifuri, baadaye akamuuliza mkewe mbona hujanipigia kura akamwambia kama mume anafaa lakini kama kiongozi hawezi, ndio maoni yake. Mama yule anasema mumewe ni mume safi lakini kwa uongozi hawezi hivyo anataka mtu anayefaa,” alisema.

Hivyo Wasira aliwataka wapiga kura ndani ya CCM wazingatie maoni ya wananchi lakini watende haki ,watumie mfano wa huyo mama na kusisitiza ni vema wakasikiliza wananchi wanasema nini juu ya nani.
Pia alisema CCM inataka watu wanaoaminiwa na wananchi sio wanaojulikana maana kuna tofauti kati ya kuaminiwa na kujulikana.”Maaana hata wezi wanajulikana, kwa hiyo tunataka wanaoaminiwa na wananchi sio wale wanaojulikana maana hata matapeli wanajulikana,” alisema.
Alisema huko nyuma kulikuwa na utaratibu wa kuwa na wapiga kura wachache hivyo kulikuwa na baadhi ya wagombea wanawatumia watu wachache wamchague, lakini kwa sasa wameongeza idadi ya wapiga kura za maoni ndani ya Chama hicho.
Hata hivyo, alisema yeye Makamu Mwenyekiti wa na ndio msimamizi wa maadili hivyo wanasema chama hicho ni cha wakulima na wafanyakazi ingawa siku hizi wakulima wamebadilika , kwani wako wakulima lakini pia wafanyakazi na wachimbaji.
Alisema katika makundi hayo wako wenye fedha na hilo si tatizo ila tatizo ni namna unavyotumia fedha kutafuta uongozi.”Hivyo tunaviuliza vikao maana mko karibu nao yeye alitumia ngapi?Hata hivyo kutakuwa na njia nyingine ya kupata habari kama walioko huku watatudanganya, tuna njia nyingi za kupita na kusema mbona huyu amefanya moja mbili tatu na hamkuvisema.
Wasira alisema ni vema wanaoshiriki vikao vya kupiga kura za wagombea wakaangalia na ndio wataamua hata kama mgombea atatoa hela angalieni wananchi wanamtaka nani.” Mkifanya hivyo mtakuwa mmekitendea haki chama hiki ambacho tumerithi kutoka kwa wazee wetu.

UCHAGUZI HURU, HAKI
Pia Wasira alisema kuwa katika kuhakikisha uchaguzi mkuu mwaka huu unakuwa huru na haki vyama vya siasa vilimshauri Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kutungwa kwa Sheria za Uchaguzi ambazo zitafanya uchaguzi uwe bora kuliko za nyuma na sheria zilishatungwa.
Alisisitiza uchaguzi mkuu utakuwa huru na wa haki na CCM itashinda na wako tayari kushindana na chama chochote na ushindi kwao ni hakika.