NanAziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Zaidi ya wanawake 50 kutoka Kata ya Keko Mwanga, Dar es Salaam, wamepatiwa mafunzo ya utengenezaji wa mbolea mboji kwa kutumia taka za majumbani, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Akizungumza na Jamhuri, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Active African Women for Research and Development (AAWORD), Hilida Swai, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanawake katika maeneo ya mabondeni ili waweze kutunza mazingira na kuzalisha mbolea ili kuongeza kipato.

“Tumeamua kutumia Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuwafundisha wanawake 50 namna ya kutengeneza mbolea salama isiyo na kemikali, kwa kutumia taka wanazozalisha majumbani ambapo itawasaidia kujiinua kiuchumi na kulinda mazingira,” amesema Hilida.

Amesema AAWORD inalenga kujenga harakati madhubuti za wanawake nchini kwa kutumia mbinu za haki za binadamu, utafiti wa vitendo na elimu ya jinsia ili kutambua na kuimarisha mchango wa mwanamke katika maendeleo ya kiuchumi na utawala wa kidemokrasia.

Hilda amesema shirika hilo lilianzishwa mwaka 2024 na mwaka huu limepata ufadhili kutoka Global Fund for Women kwa ajili ya kutekeleza mradi wa mabadiliko ya tabianchi unaoangazia athari kwa wanawake wanaoishi maeneo ya mabondeni.

“Waathirika wakubwa wa uchafuzi wa maji na mazingira ni wanawake, kwa sababu wanatumia maji katika shughuli nyingi za kifamilia. hivyo tumeamua kuwajengea uwezo ili wawe sehemu ya suluhisho,” amesema.

Aliongeza kuwa wanawake wa Keko Mwanga A na B wameingizwa kwenye kamati mbalimbali za uhamasishaji mazingira ili kuhakikisha miradi ya utunzaji wa mazingira na usalama wa kaya inatekelezwa kikamilifu.

Amedai kupitia maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, shirika hilo lilitoa mafunzo ya uchechemuzi wa kupinga ukatili sambamba na elimu ya utengenezaji wa mboji, ili kuwawezesha wanawake kupata kipato na kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira.

“Mazingira yakiharibika, waathirika wakuu ni wanawake na watoto,tunataka wanawake wawe vinara wa utunzaji wa mazingira kwa sababu mazingira mazuri yanapunguza magonjwa na kuongeza usalama wa jamii,” amesema Hilida.

Hilda amesema mkakati wa mwaka ujao ni kupanua wigo wa mradi katika maeneo mengine ya mabondeni nje ya Keko Mwanga, ili kuongeza idadi ya wanawake wanaonufaika na mbinu za kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Rehema Mwaseba, mwezeshaji wa somo la uzalishaji mboji, amesema utengenezaji wa mbolea hauhitaji eneo kubwa wala gharama kubwa, bali umakini katika kuchagua na kutenganisha taka zinazooza.

“Mwanamke akiwa na vifaa vya msingi kama ndoo, mapipa, majani makavu, majani ya ndizi, majivu, udongo na samadi, anaweza kuzalisha mbolea ndani ya wiki 10. Mbolea hii salama inaweza kumpatia kipato na kumwezesha kujitegemea kiuchumi,” amesema Rehema.

Rehema ameongeza kuwa mbolea hiyo haina kemikali na ni salama kwa matumizi ya kilimo, hivyo kusaidia kaya nyingi kuboresha bustani na mashamba ya mboga mboga.