Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Diwani Mteule wa Kata ya Pangani, John Katele, ni miongoni mwa madiwani wanne waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Meya wa Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wengine waliopata fomu ni Diwani Mteule wa Kata ya Tumbi, Dkt. Mawazo Nicas, Mashaka Mahande wa Kata ya Sofu na Elinius Mapunda.
Akizungumzia mchakato huo, Kaimu Katibu wa CCM Kibaha Mjini, Latifa Semwanza, alisema utoaji wa fomu ulianza Novemba 20 na kukamilika rasmi, na sasa chama kinaendelea na vikao vya mchujo kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi wa ndani.
Aidha, Semwanza aliwataja waliochukua fomu za kuwania nafasi ya Naibu Meya kuwa ni Ally Simba wa Kata ya Misugusugu, Aziza Mruma (Viti Maalum) na Ramadhani Lutambi wa Kata ya Mailimoja
“Chama cha Mapinduzi kinawapongeza wote waliopata fomu, na kinawaomba wagombea pamoja na wanachama kuendelea kuwa wavumilivu na watii wa kanuni za uchaguzi, wakati mchakato wa ndani ukiendelea ili kupata viongozi kwa maslahi ya maendeleo ya wananchi,” alisema Semwanza.



