Na Dk Reubeni Lumbagala, JamhuriMedia, Tanga
Ni takwa la kisheria kwa waombaji wa mikopo ya elimu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwa na namba ya utambulisho (National Identification Number-NIN) au kitambulisho cha uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuweza kuomba mikopo ya elimu.
Pamoja na kwamba takwa hilo la kisheria kwa miaka ya nyuma kwa mwombaji ambaye hakuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia aliweza kuomba na kupata mkopo, lakini kwa mwaka huu wa masomo wa 2025/2026, bila namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia, mwombaji atashindwa kuomba mkopo na hivyo kukosa mkopo.
Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa walifanya mkutano Mei 16, 2025 ambapo mkazo juu ya kila mwombaji wa mkopo wa elimu kuhakikisha ana namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia uliwekwa bayana mbele ya vyombo vya habari na Watanzania kwa ujumla.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia alisisitiza juu ya umuhimu wa waombaji kuwa na namba ya NIN. “NIN itaiwezesha HESLB kuwa na taarifa sahihi na za kipekee za kila mwanafunzi. Kwa kutumia NIN kutatuwezesha kuboresha uwezo wetu wa kufuatilia wanufaika waliokopeshwa baada ya kuhitimu.
Tumeunganisha mifumo yetu ili kuwezesha kuhakiki taarifa za waombaji mikopo kupitia NIN. Tayari wataalamu wa Tehama kutoka pande zote mbili (HESLB na NIDA) wanashirikiana kuhakikisha mifumo yetu iliyounganishwa inafanya kazi kwa ufanisi,” amesema Dk. Kiwia.
Kimsingi, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikisisitiza mifumo ya serikali kusomana ili kurahisisha utendajikazi na ufuatiliaji kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Kabla ya maboresho makubwa yaliyofanywa na HESLB kuhusiana na mifumo ya kidigitali, kulikuwa na changamoto ya kupata taarifa za wanufaika wahitimu ambao hawajarejesha mikopo ambayo ni fedha zilizotumika kuwasomesha elimu ya juu katika taasisi mbalimbali za elimu.

Kwahiyo, maboresho makubwa yamefanyika kwa HESLB kuungana na taasisi nyingine mbalimbali ili kuwa na mfumo wa pamoja ambao utarahisisha utendajikazi na ufuatiliaji. Sambamba na hilo, kwa kuzingatia gharama zilizopo katika elimu ya kati na ya juu yaani ada, chakula, malazi, vitabu, kudurufu matini (kutoa photocopy), mafunzo kwa vitendo; Watanzania wengi wanahitaji kuwezeshwa kifedha kupitia mikopo inayoratibiwa na HESLB.
Hivyo, niwashauri waombaji wa mikopo ambao hadi sasa hawana namba ya NIN kuomba namba hizo kupitia tovuti ya NIDA au kwenda kwenye ofisi za NIDA zilizopo katika Halmashauri na wilaya zao ili kupata namba ili kuweza kuomba mikopo pindi dirisha la maombi ya mikopo litakapofunguliwa rasmi na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kupata mikopo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema NIDA wapo tayari kuwahudumia waombaji wa mikopo. “Tunafurahia wenzetu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wameona na kutambua jitihada zetu, pamoja na mambo mengine watatuunga mkono katika kutoa hamasa hii kwa vijana. Namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) inapatikana ndani ya siku 5 baada ya kujisajili, na kadi ya NIDA inapatikana ndani ya siku 21 baada ya uthibitisho wa taarifa za mwombaji, hakikisha unapojisajili unapata kadi,” amesema.

Dirisha la maombi ya mikopo linatarajiwa kufunguliwa mwezi Juni, 2025, ni vyema waombaji watarajiwa wasiokuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia wakaanza kufuatilia mapema badala ya kusubiri hadi muda wa kuomba mkopo ufike ndipo waanze kuhangaika kufuatilia. Ikumbukwe kuwa bila namba ya utambulisho, maombi ya mikopo hayataweza kukamilika.
“Tunatarajia kufungua dirisha la maombi ya mikopo mwezi Juni, 2025, kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026, namba ya utambulisho wa Taifa itakuwa hitaji la lazima katika kujaza fomu za maombi ya mikopo, hivyo waombaji wote wanapaswa kuwa na namba hii wakati wa kujaza maombi yao ya mkopo,” alisisitiza Dk. Kiwia.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.



Maoni: 0620 800 462.