Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Mwanza
Jana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanzisha rasmi mchakato wa uchaguzi katika ngazi ya wabunge na madiwani kwa kuteua majina ya wanachama wake watakaopiga goti mbele ya wajumbe kuomba kura.
Mchujo utakaofanyika wiki ijayo unalenga kupata maoni ya wapigakura kwa njia ya uwakilishi juu ya nani anafaa kuwa mgombea ubunge au udiwani kwa majimbo na kata zote nchini.
Sitanii, joto ni kubwa katika maeneo mbalimbali nchini. Nimeona hata baadhi ya watendaji wa serikali wakiishiwa pumzi na kuamua kutema nyongo baada ya kuhusishwa na kukata majina ya wagombea wa viti maalumu. Kwenye majimbo ndiko usiseme. Watu wanaojifanya wanaweza kubadili mchezo tayari wamevuna mamilioni.
Wanawaingiza ‘mjini’ wagombea kwa kuwaambia majina yao yalikatwa katika ngazi ya wilaya wakatumia nguvu yakafika mkoani. Wengine wanaambiwa yalikatwa mkoani, wakatumia nguvu kuyafikisha Kamati Kuu. Hizo zote ukizisikiliza ni dalili kuwa wavujishaji wa taaifa hizo ambazo aghalabu ni feki, wanajitengenezea mazingira ya kuvuta chochote kutoka kwa wagombea.
Sitanii, nilisubiri niandike makala hii baada ya majina kutangazwa, lakini kwa muda unavyokwenda na kwa gazeti la wiki, nitakuwa sitendi haki gazeti likishindwa kwenda kiwandani, kwa kuwa ninasubiri majina. Nafahamu fukuto lililotokana na uteuzi wa mwaka 2020. Walioamini wanakubalika kwani waliongoza kura za maoni wakakatwa, zamu hii wamerudisha majina yao kwa kishindo.

Nafahamu kuwa baadhi ya waliopita kwa ‘goli la mkono’ wachache wamekuwa wabunge wazuri sana kwa kutetea maendeleo ya majimbo yao, lakini wengi wameishi katika kivuli cha chuki. Miaka mitano yote imekwisha wakilumbana na kutambiana. Kwa kweli yapo majimbo ambayo hao waliopita kwa goli la mkono leo hawana cha kuonyesha.
Miaka mitano wameitumia kufanya malumbano na waliokuwa washindani wao, kumbe hawakujua kuwa mwaka huu Oktoba 29, watapaswa kuwa na cha kuonyesha kwa wapigakura. Hawa sasa wanapumulia mashine. Orodha hii ya majina baada ya kutangazwa ama wakajikuta wamo au hawamo, sasa wanaanza safari mpya ya kusaka mchawi.
Sitanii, kwenu wapigakura za wajumbe. Wagombea hawa walioletwa mbele yenu mnayo nafasi ya kuwauliza, mtatufanyia nini? Waulizeni kama majimbo yenu au kata zenu zina maji, umeme, taa za barabarani, shule nzuri, barabara za lami, vituo vya afya, viwanja vimepimwa, hakuna migogoro ya ardhi, viwanja vya wazi havijavamiwa (kwa maeneo ya mijini), soko la mazao mlipo linapatikana, huduma zinatolewa katika ofisi za umma bila kudaiwa rushwa.
Waulizeni hawa wanaoomba ubunge na udiwani kama wao na watumishi wa umma walioko chini yao si miungu watu. Ulizeni ulinzi na usalama wenu ukoje. Kuku, mbuzi na ng’ombe hawaibiwi? Ukisahau shati nje au kitenge umefua asubuhi unavikuta? Majirani wanaopanga katika nyumba za eneo lenu mnafahamiana? Mna ushirikiano katika shida na raha?
Waulizeni kuhusu suala la ajira likoje? Ilani ya CCM imetangaza kujenga kongani za viwanda kila wilaya, ambayo hiki ni chanzo kikuu cha ajira. Waulizeni wabunge wenu kwenye wilaya yenu wamevutia au wana mpango wa kuvutia viwanda vingapi kati ya viwanda 45,000 vilivyojengwa nchini? Kataeni kanga, kofia, vitenge, pombe, ubwabwa kama vishawishi vya kuwapigia kura.
Sitanii, maswali haya niliyopendekeza na mengine mengi wakija kwenye mikutano ya kampeni, mkiyauliza atakayeyajibu kwa ufasaha na mwisho wa siku akashinda, mtakuwa mmeingia naye mkataba wa kuleta maendeleo. Mkimchagua mgombea kwa sababu ametoa wali na kinywaji, baada ya Oktoba 29, 2025 nitasikia kelele za mbunge au diwani wetu hatufai zinaanza tena. Tusifanye kosa. Tuchague maendeleo, si vitita vya rushwa. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827