Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media- BUNDA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, ametoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya kikundi cha watu wachache wanaoleta chokochoko katika mitandao ya kijamii wanaotaka kuvuruga amani.


Amesema kikundi hicho ni miongoni mwa watu wachache wasioridhika, hata hivyo kamwe hawatotimiza dhamira yao ovu.


Wasira ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi wa urais, wabunge na madiwani mjini Bunda Leo Oktoba 9,2025.


Amesema amani na utulivu utaendelea kutawala nchini kama ilivyo siku zote
“Kuna chokochoko nyingi ambazo hazipo kwa watu, zipo kwa wacheche wanaotumia mitandao ya kijamii. Naomba msome ile mitandao kwa makini, kuna watu hawaridhiki.


“Kinamama wanaopika maharage wanafahamu yapo maharage hata ukiyapika vipi yatatokea machache yakielea. Hayo hayaivi na ndiyo watu wanaosumbua,”amesema
“Watu hao hawawezi kuisumbua nchi, namwambia mgombea wetu (Dk. Samia) asibabaishwe na watu hao wachache, hata ukifanya vizuri namna gani wao wananuna, ndivyo walivyo.”


“Wapo watakaokumbuka kwa wema wenye nia njema. Dk. Samia amefanyakazi kubwa, jinsi mnavyomuunga mkono hapa ndivyo anavyoungwa mkono Tanzania nzima,” alieleza.


Amesema CCM imewaletea mgombea urais mwenye mafanikio makubwa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi iliyopita na siyo mwenye uwezo mdogo.


“Hatuwaletei mgombea urais ‘lena’ tunawaletea mgombea urais aliye fanyakazi ya urais kwa mafanikio makubwa,” alisisitiza.

Amesema Rais Samia aliingia madarakani katika misukosuko mikubwa wakati ambao taifa lilikumbwa na ugonjwa wa Uviko-19, kufariki dunia kwa Rais aliyekuwa madarakani (Hayati Dk. John Magufuli) na kushuka kwa uchumi.

Amesema alipoingia madarakani alitumia maneno mawili ambayo ni ‘Kazi Iendelee’.
“Alipewa mtihani mkubwa aliachiwa miradi mikubwa ya nchi yetu. Aliachiwa reli haijakamilika leo imekamilika mpaka Makutupora ya Singida kilometa 722 kutoka Dar es Salaam.


“Aliachiwa bwawa la Mwalimu Nyerere lilikuwa chini ya asilmia 30, hata hivyo asilimia 70 imejengwa chini ya usimamizi wa Rais Samia na Tanzania ina umeme wa kutosha,” alibainisha.


Kuhusu elimu elimu katika Wilaya ya Bunda, Rais Samia amejenga shule mpya 13 za msingi, shule 15 za sekondari, zahanati 20, vituo vitatu vya afya na hospitali moja mpya.


Amesema ametoa mchango mkubwa kupunguza vifo vya kinamama na watoto kwa kuwa alipoingia madarakani alikuta katika kila vizazi hai 100,000 vizazi 500 walifariki dunia kila mwaka.


Amesema Samia amewezesha kushusha hali hiyo ambapo sasa katika kila vizazi hai 100,000 mia tano walikuwa wakifarkki leo vimeshuka kufikia 100.


Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, amesema alipokabidhiwa Wizara ya Maji, alipewa maagizo na Dk. Samia kuhakikisha hakuna mwanamke atakayeteseka kwa kukosa maji.

Alisema hali ya maji miaka minne iliyopita katika wilaya hiyo ilikuwa mbaya kwa kuwa miradi iligeuka kichaka cha watu kufanya ubadhirifu.

Aweso amesema Samia alimwagiza kufika wilayani Bunda kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo huku akitoa sh. bilioni 10 kutekeleza mradi wa maji Nyabeho.

Alisema mradi huo umeshakamilika, wananchi wanapata maji safi na salama.

“Hapa tuna miradi mingi ambayo ipo ilikamilika na mengine ipo hatua mbalimbali kwa gharama ya sh. bilioni 20. Zaidi ya wananchi asilimia 87 eneo la Bunda Mjini wanapata huduma ya maji,” alieleza.


Amesema maeneo yaliyokuwa na changamoto ya maji ni vijijini ambapo Dk. Samia amechukua hatua kuhakikisha huduma hiyo inapatikana.


Amesema ametoa fedha zaidi ya sh. bilioni 100 kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Bunda na Tarime na kumaliza tatizo hilo.