Na Mwandishi Wetu, Katoro
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema tangu kupata uhuru Tanzania imepata maendeleo makubwa na kwamba wanaosema hakuna kilichofanyika ni vema wakafanya utafiti kwanza badala ya kuwa kama kasuku kukariri maneno wasiyoyajua.
Wasira ameyasema hayo jana alipokuwa akizingumza na wana CCM katika mkutano wa hadhara Katoro, mkoani Geita akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama mkoani humo ambapo pia alifanya vikao vya ndani.
Akieleza kuhusu maendeleo yaliyofanyika nchini tangu kupatikana kwa uhuru alisema ni makubwa na wenye umri mkubwa wanajua vizuri nchi ilivyokuwa na wamekuwa wakishuhudia hatua mbalimbali zinazofanywa na serikali inayoundwa na CCM.
“Labda ninyi vijana hamwelewi lakini niwaambie wakoloni wa Kijerumani na wakoloni wa Kiingereza wamekaa Tanganyika miaka 75, Wajerumani wamekaa miaka 35, wamejenga reli kwa viboko bila malipo. Waingereza wamekaa miaka 40 walitumwa na Umoja wa Mataifa (UN) watuendeleze tujitawalie, lakini miaka 40 ya Waingereza wametuacha na wahandisi wawili katika nchi isiyo na barabara.
“Wametuachia nchi hakuna daktari hata mmoja, walikuwepo madaktari kutoka India na Pakistani nao walikuwa Dar es Salaam. Wakati tunapata uhuru akina mama walikuwa hawajifungui ila wanazaa maana hakukua na kliniki, hivyo walikuwa wanazaa kama ng’ombe anavyozaa ndama. Ng’ombe umeona wapi ana kliniki (ya uzazi)? Hiyo ndio hali waliyotuacha nayo (wakoloni) wametuacha hatuna barabara.
“Leo anakuja mtu hajafikisha umri wa miaka 30 au miaka 40 anawaambia hakuna maendeleo. Wewe uliwahi kutembea kwa miguu…hao wanaosema hakuna maendeleo ambayo yamefanyika akija muulizeni hivi kwako maendeleo ni kitu gani?” alieleza.
Wasira alisema inawezakana wanaosema hakuna kilichofanyika wanazungumza kama kasuku ambaye anakariri tu haelewi hata maana ya maneno anayosema na kwamba hao ndio wanasiasa wapya, “sisi tumejitawala tulikuwa na msomi mmoja tu mwenye ‘Master degree’ (shahada ya uzamili), Julius Nyerere, ndiye alikuwa ameandaliwa na wakoloni kwa miaka 75.
“Leo wala sio Tanganyika nilikuwa namuuliza mkurugenzi wa Bukombe asubuhi anasema ana wahandisi 12, nikasema wewe ni tajiri kuliko Tanganyika ya mwaka 1970 maana kulikuwa na wahandisi wawili wewe unao 12. Namuuliza madaktari anasema wengi tu sisi hatukuwa na daktari.
“Hiyo ndio nchi tuliyorithi, leo unaweza kwenda mkoa wowote wa Tanzania kwa lami. Zamani wakati tunakabidhiwa nchi lami ilikuwa inatoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa sababu kulikuwa na wazungu wanalima mkonge, ilikuwa inatoka Tanga mpaka Korogwe kwa sababu kulikuwa na wazungu wanalima mkonge.
“Wazungu walikuwa wanalima kahawa, kwa hiyo kukawa na barabara ya wazungu wanatoka mashamabani wanawahi majumbani, ndio nchi tuliyorithi kutoka kwa wakoloni halafu leo unapita unawaambia wananchi hakuna maendeleo, wewe ni kasuku unazungumza mambo bila utafiti, hulewi nchi hii tumeitoa wapi?”
ATAJA KAZI NNE ZA CCM
Katika hatua nyingine, Wasira alitumia nafasi hiyo kufafanua mambo manne muhimu ambayo Chama kitaendelea kuyatekeleza kwa nguvu zote kwa mustakabali wa taifa.
Alisema jambo la kwanza ambalo CCM itaendelea kusimamia kwa nguvu zote ni umoja na mshikamano wa Watanzania ambapo alifafanua msingi wa umoja una mkono wa watu ambao tayari wametangulia mbele ya haki.
“Kuna wazee nyuma yetu ambao wametangulia mbele ya haki wametuachia kazi hiyo tuiendeleze, wapo wazee kama Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Abeid Aman Karume ambaye alikubali kuacha urais wa nchi yake awe Makamu wa Rais kwa sababu ya umoja wa taifa.
“Hiyo ndio kazi ya kwanza ya chama chetu kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa moja na watu wetu, wanaishi kwa amani na wanatoa mchango wao kwa maendeleo ya nchi yao bila ubaguzi. Kazi ya kudumu kwa chama cha kudumu.”
Wasira alitaja jambo la pili muhimu kwa Chama ni kusimamia amani iliyopo na kueleza kuwa hivi sasa kuna baadhi ya watu wanachezea amani iliyopo ikiwemo kupanga kuvunja Katiba wazuie uchaguzi.
“Amani inapotoweka wanaoteseka ni akina mama, watoto na wazee. Wanaochezea amani yetu watakuja hapa wawaambie muwaunge mkono katika kuondoa amani ya Tanzania. Nchi ikiwa haina amani mtakimbilia wapi. Msikubali kuvunja amani yetu.”
Wasira alisema CCM iko imara katika kuhakikisha amani inaendelea na kutoa mfano Mkoa wa Geita ikiwemo Katoro ni wafanyabiashara na wachimbaji wa madini, amani itakapokosekana hakuna biashara ambazo wanaweza kufanya.
Alisema amani nchini ni jambo la msingi na kwamba CCM imeahidi kuwa ajenda ya kudumu ambayo itaendelea kusimamiwa na Chama cha kudumu (CCM).
Aliwaeleza wananchi hao kuwa, yeyote anayewaambia wamuunge mkono kuchukua hatua ambazo ni kinyume na Katiba wakate. “Ninawaambia ajenda ya amani ni ajenda yetu, tena ni ajenda ya kudumu kwa chama cha kudumu.”
Jambo la tatu alisema ni CCM kuendeleza uhuru wa taifa kwa kuwa ndio unasaidia kufanya uamuzi na kufafanua kuwa wananchi waliudai ili kuamua mambo yao wakiwa huru.
“Uhuru wa kutukanana ni uhuru mpya na haueleweki, nchi gani ambayo watu wake wanatukanana badala ya kujadiliana, wanatukanana katika mitandao, tulidai uhuru kwa sababu mambo ambayo tunafanya leo tusingeweza kuyafanya wakati wa ukoloni. Chama cha TANU na Afro Shiraz Party wametukabidhi mkoba wa kuendeleza uhuru, hivyo CCM tunayo kazi ya kuulinda uhuru wetu.
Alitaja jambo la nne ni kuendelea kuleta maendeleo ya Watanzania na katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa, nzuri katika kusimamia maendeleo.
“CCM tutaendelea kusimamia upatikanaji wa maendeleo ya wananchi katika maeneo yote. Chini ya Rais Samia tumeshuhudia maendeleo makubwa yamefanyika, utekelezaji wa miradi umefanyika kwa asilimia 100. Rais Samia amekamilisha ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo mtangulizi wake Dk. John Magufuli aliacha ujenzi ukiwa asilimia 34, lakini sasa limekamilika kwa asilimia 100 .
“Pia Rais Samia ameendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya SGR (Reli ya Kiwango cha Kimataifa) ambayo kwa sasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma inamekamilika na inatoa huduma, lakini ujenzi umefika Makotopola mkoani Singida, pia kuelekea Tabora, Shinyanga mpaka Mwanza ujenzi unaendelea. Daraja la Kigongo-Busisi nao umekamilika na Rais Samia atazindua daraha hilo kesho (leo). Hivyo kuleta maendeleo ni kazi ya kudumu ya CCM,” alieleza.


