Serikali inaratibu Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, kwa lengo la kukuza ujuzi wa nguvukazi ya taifa ili kumudu ushindani katika soko la Ajira ambapo hadi sasa Watanzania 168,657 wamenufaika.  

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Latifa Juwakali lililouliza Je, Serikali ina mkakati gani wa kukuza vipaji na ujuzi wa vijana wa Tanzania?

Akijibu swali hilo, Mhe. Rahma amesema Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ina lengo la kuwezesha nguvukazi kuwa na ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira ili waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Amesema, Programu hiyo inatekelezwa kupitia maeneo manne ambayo ni kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi, kukuza ujuzi kwa wafanyakazi, mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu na mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.