Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIKA kuadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika, Watanzania wametakiwa kukumbuka siku hiyo kwa misingi ya haki, amani, mshikamano na umoja wa kitaifa, huku wakiepuka mivutano yoyote inayoweza kugawanya taifa, ikiwemo migawanyiko ya kidini, kikabila au kisiasa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Everlasting Legal Aid Foundation, Dkt. Khamis Masoud, amesema kuwa kumbukizi ya uhuru inapaswa kuwa fursa ya kuimarisha mshikamano na kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali tofauti zao.

Dkt. Masoud amesema ni muhimu viongozi wa dini na serikali kuungana katika kuhubiri amani, heshima na ustahimilivu, kwa kuwa wao ni nguzo muhimu katika kuunganisha jamii.

“Ni muhimu viongozi wa dini kutazama namna bora ya kuwaleta wananchi pamoja kuhusu amani badala ya kufanya mambo yanayoweza kugawanya taifa kwa mitazamo ya kidini,” amesema Dkt. Masoud.

Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wa serikali wanapaswa kuwa wazalendo na wenye uthubutu wa kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya taifa. Ameongeza kuwa hata pale ambapo ni lazima, viongozi hao wanapaswa kuwa tayari kung’atuka madarakani ili kulinda amani, mshikamano na haki nchini.

Mbali na hayo, Dkt. Masoud amebainisha umuhimu wa kuimarisha diplomasia na mahusiano ya kimataifa, akieleza kuwa Tanzania inahitaji uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali ili kuendeleza maendeleo na uchumi wa nchi.

Ameitaka serikali kuendelea kumuunga mkono Rais katika utekelezaji wa mikakati ya kidiplomasia yenye manufaa kwa taifa.

Itakumbukwa kuwa kwa mwaka 2025, serikali iliahirisha sherehe za maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika, na kuelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kutumika katika sherehe hizo kufadhili ukarabati wa miundombinu iliyoathiriwa na vurugu za uchaguzi mkuu zilizotokea Oktoba 29, 2026.