Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali imesema inafanya jitihada za kuwarejesha nyumbani Watanzania wote waliopo Israel na Iran ili kuwaepusha na mashambulio yanayoendelea baina ya mataifa hayo mawili ya Mashariki ya Kati.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana kuhusu hali ya Watanzania waliopo Israel na Iran, ilitaja idadi ya raia waliopo Iran kuwa ni 168 wakiwamo wanafunzi 134 katika mji wa Qom na wengine 34 jijini Tehran.
“Kwa upande wa Israel, inakadiriwa kuwa kuna zaidi ya Watanzania 200 wakiwamo watumishi wa Ubalozi wa Tanzania, wanafunzi na wafanyakazi katika taasisi mbalimbali, kati yao, Watanzania 50 tayari wamejiandikisha kwa ajili ya kupatiwa msaada wa kurejea nyumbani,” ilieleza taarifa ya wizara.
Serikali ilisema inawahakikishia usalama Watanzania wote waliopo katika mataifa hayo mawili, na kutoa mwito kwa Watanzania wengine ambao hawajajiandikisha wafike katika nchi za Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kuwait na Israel na kujiandikisha.
“Balozi zetu nchini Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuwa zikiwasiliana na Watanzania waliopo katika maeneo ya Iran na Israel, zikiwataka kuchukua tahadhari za kiusalama, wakati serikali ikiendelea kushughulikia masuala yanayohusu usalama wao ikiwa ni pamoja na mustakabali wao wa kurudi nyumbani,” ilieleza taarifa hiyo.
Vita inayoendelea kati ya Taifa la Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza Juni 13, mwaka huu na mpaka sasa mataifa mbalimbali yakiwamo Australia, China, India, Japan na Pakistan yameanza kuwasaidia raia wake kuondoka katika mataifa hayo.
