Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka baadhi ya wananchi wanaopotosha kuhusu Muungano kuacha vitendo na badala yake waulinde na kuuenzi kwani umeleta manufaa makubwa.
Ametoa wito huo bungeni jijini Dodoma leo Mei 26, 2025 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi aliyetaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu kuwepo kwa wimbi la upotoshaji wa Muungano.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis amesema pamoja na hatua mbalimbali Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo vyombo habari.

“Kuna watu wanapotosha kuhusu chimbuko, maendeleo na ukweli kuhusu Muungano huu, niwaambie tu wananchi waache kubeza Muungano kwani hapa tulipo ni kwasababu ya nguvu kubwa ya Muungano huu,” alisema.
Hivyo, kutokana na changamoto hiyo ya baadhi ya wananchi kutofikiwa na elimu hiyo, alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imechukua hatua ya kutoa elimu kupitia makongamano, vipindi vya redio na televisheni ili wananchi wafahamu ukweli kuhusu Muungano huu adhimu.
Aidha, Mhe. Khamis akijibu swali Mbunge huyo kuhusu taasisi ngapi zimefungua ofisi zake Zanzibar, alisema kuwa jumla ya taasisi za Muungano 33 zimefungua ofisi na kuanza kutoa huduma kwa upande wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.
Alitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nyinginezo.
Awali, Naibu Waziri Khamis alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimeweka utaratibu wa kutatua changamoto hizo kupitia mfumo rasmi wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la msingi la Mhe. Maryam aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kumaliza kero za Muungano zilizobaki ikizingatiwa kuwa imefanya kazi kubwa hadi kubakiza kero nne.
Akiendelea kujibu swali hilo alisema lengo la vikao hivi ni kuhakikisha changamoto zote zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza changamoto 22 kati ya 25 zilizoibuliwa tangu mwaka 2006.
Alisema Serikali zote mbili zinaendelea kuratibu vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ambapo Kikao cha Kamati hiyo kilifanyika Aprili 4, 2025 Ikulu Dar-es Salaam kujadili hoja nne za Muungano zilizosalia na hatua mbalimbali za utatuzi zinaendelea.