Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
ZAIDI ya watu 200 wamenufaika na uchunguzi wa kisukari bure uliofanywa na hospitali ya Shifaa ya Kinondoni jijijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kisukari duniani
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Emmanuel Maganga wakati akizungumza kuhusu uchunguzi wa maradhi ya kisukari yaliyofanywa bila malipo hospitalini hapo.

Alisema ugonjwa wa kisukari usipotibiwa vizuri unaweza kusababisha matatizo ya figo, macho misuli na watu wengine kupata vidonda visivyopona na kusababisha kukatwa baadhi ya viungo kuokoa uhai wao.
Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaosafisha figo Dialysis hali ambayo inasababishwa na wagonjwa wa kisukari kushindwa kupata huduma sahihi na za kibingwa kwa wakati.
“Haya yote ndiyo yamesababisha hospitali ya Shifaa kufungua kitengo ambacho matibabu yote yanayohusiana na kisukari yatapatikana sehemu moja kama lishe mazoezi, macho, na ushauri wa kupunguza uzito uliokithiri, kwenye kitengo hiki hapa tunatoa pia upasuaji wa kupunguza uzito,” alisema.

“Kwa kweli wananchi waliofika hapa Shifaa wamepata huduma nzuri na wamepata ushauri kuhusu lishe kupunguza uzito na kwa kweli wamefurahi sana kwa hiyo wito wangu tupambane tusipate kisukari na atakayepata basi apate huduma iliyo sahihi na mapema,” alisema
Naye Daktari bingwa wa macho wa hospitali hiyo, Jacqueline Mchilla alisema ugonjwa wa sukari unauhusiano wa moja kwa moja na matatizo ya macho kwani ni kawaida kwa sukari kuathiri mishipa ya fahamu.
Alisema sukari pia imekuwa ikiathiri mishipa ya fahamu kwenye ubongo hali ambayo wakati mwingine husababisha wagonjwa husika kupata stroke.

“Mgonjwa yoyote wa sukari anashauriwa kumwona daktari mara kwa mara kwasababu sukari ikishaingia kwenye macho ikaathiri mishipa ya fahamu kwenye macho inasababisha upofu na ikishafika wakati huo ni ngumu kurejesha uoni kamili,” alisema Dk Jacqueline
“Sisi madaktari tunashauri kwamba ni vizuri wananchi wakajikinga zaidi kabla ya kupata madhara kwasababu kadri sukari inavyoongezeka na tatizo la kuona linazidi kuwa kubwa kwa hiyo tubadili mtindo wa maisha kuepuka maradhi haya ,” alisema


