Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Watu 232 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa muda wa siku tatu katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba).

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasilaino wa Taasisi hiyo Anna Nkinda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma zinazotolewa na JKCI katika maonesho hayo.

Anna alisema huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ni pamoja na kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo, vipimo vya kuangalia wingi wa sukari kwenye damu na kuangalia shinikizo la juu la damu.

Afisa Uuguzi wa chumba cha upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nyamtacho Senteuh akiwafundisha watoto waliotembelea banda la Taasisi hiyo jinsi moyo unavyofanya kazi wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

“Vipimo vingine vingine vinavyotolewa katika banda letu ni kipimo cha kuangalia kiwango cha mafuta mwilini, kipimo cha kuangalia utendaji kazi wa figo na ini, kipimo cha kuangali kiwango cha madini chumvi mwilini pamoja na elimu ya lishe, matumizi sahihi ya dawa na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza”. 

“Katika banda letu pia tunafanya maonesho ya vifaa mbalimbali vya matibabu ya moyo tunavyovitumia kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hii ikiwa ni pamoja na valvu za moyo na betri za moyo (Pacemaker)”, alisema Anna.

Msemaji huyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema wanatoa pia elimu ya jinsi ya kumuhudumia mgonjwa wa dharura  pamoja na kuonesha teknolojia ya matibabu kwa njia ya mtandao kwa kutumia kifaa cha DOZEE.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo walifurahi kwa huduma walizozipata na kuiomba Taasisi hiyo kuendelea kuwafikia na kuwapa huduma hizo za kibingwa mara kwa mara.

Sara Mkoni mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam alisema imekuwa kawaida yake kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kila msimu wa maonesho ya Sabasaba kwani anapata huduma kirahisi na kwa haraka.

“Nimekuwa nikitembelea maonesho ya Sabasaba kila mwaka tena nawahi siku za mwanzo ili niweze kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika banda hili, nawaomba muendelee kutuhudumia kila mwaka bila kutuchoka”, alisema Sara.

Daktari wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ahmed Mchina akimfundisha mtoto aliyetembelea banda la Taasisi hiyo namna ya kutoa huduma ya kwanza wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Sara aliwasihi wananchi wanapotembelea maonesho hayo wasiishie kununua vitu na kuangalia wanyama bali watumie muda wao pia kutembelea banda la JKCI na kufanya uchunguzi wa afya kwani wataalamu wa afya wanashauri kufanya vipimo mara kwa mara na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Naye Osman Maulid mkazi wa Temeke alisema maonesho ya Sabasaba kuhusisha utoaji wa huduma tofauti zikiwemo za matibabu ya moyo kunawasaidia wananchi kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa afya zao.

Osman alisema anajisikia furaha kupima moyo wake na kupata ushauri wa daktari wa lishe, ushauri ambao ataufanyia kazi ili aweze kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

Mjumbe kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Heat Team Africa Foundation (HTAF) Irene Mbonde akipokea fedha za kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo  ya moyo zilizotolewa na mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).